|
MAADHIMISHO YA MIAKA 30 YA CCM
Halmashauri Kuu ya Taifa iliyokaa tarehe 21-22
Desemba, 2006 iliamua
Matembezi ya Mshikamano yafufuliwe upya kama yalivyokuwa yanafanyika
miaka
ya 1988/92 kabla ya ujio wa vyama vingi vya siasa nchini.
Vile vile kikao hicho cha NEC kiliamua kwamba Matembezi ya
Mshikamano
yatafanyika kila mwaka sambamba na sherehe ya kuadhimisha Kuzaliwa
kwa
CCM, sherehe ambayo hufanyika tarehe 5 Februari ya mwaka unaohusika.
Kwa mwaka 2007, NEC iliamua kwamba katika vituo vyote vya Matembezi
ya
Mshikamano, kiongozi pekee wa Chama atakayedhaminiwa ni Mwenyekiti
wa CCM,
Ndugu Jakaya Mrisho Kikwete.
Walezi wa Mikoa na Viongozi wengine wa Kitaifa wamepangwa kuwa
wageni
rasmi kwenye Matembezi ya Mshikamano yatakayofanyika tarehe 4/2/2007
kuanzia saa 12.00 asubuhi katika kila mkoa. Sherehe za kuadhimisha
miaka
30 ya CCM nazo zitafanyika tarehe 4.2.2007 ambayo ni siku ya
Jumapili, ili
wanachama, wapenzi na wakereketwa wa CCM waweze kupata fursa ya
kushiriki
katika maadhimisho hayo.
Matembezi ya Mshikamano yatakayoanzia Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya
CCM
Lumumba, yatapitia barabara ya Morogoro, Msimbazi, Uhuru, Bibi Titi
na
kuishia Viwanja vya Mnazi Mmoja. Mgeni rasmi kwenye Matembezi haya
atakuwa
Mwenyekiti wa CCM, Ndugu Jakaya Mrisho Kikwete.
Chama Cha Mapinduzi kingependa pia kuchukua fursa
hii kutoa maelezo na
ufafanuzi kuhusu falsafa na sera zake. Tumeona umuhimu wa kutoa
maelezo
sahihi ili kuepusha upotoshwaji uliokusudiwa kufanywa na gazeti la
Tanzania Daima, Toleo Na. 786 la Jumapili Januari 28,2007.
Kwanza CCM kinatamka kuwa habari zilizoandikwa katika gazeti hilo
kuhusu
falsafa za CCM siyo sahihi na zinapotosha.
CCM kina historia ndefu iliyojengeka katika misingi imara kwa
kuzingatia
Katiba yake, Kanuni na Taratibu. Ni kupitia utaratibu huo, ndipo
ilipobuniwa falsafa ya Ujamaa na Kujitegemea.
CCM kama Chama cha Siasa hutoa maamuzi yake kupitia vikao rasmi kwa
mujibu
wa Katiba, Kanuni na Taratibu. Ni kwa utaratibu huu na kwa
kuzingatia
kanuni ya wakati na mahali, CCM huchambua sera zake na kuziwekea
utaratibu
wa utekelezaji. Katika utaratibu huu CCM kina sera za Msingi na sera
za
Mpito. Sera za Msingi huzingatia Lengo la CCM na sera za Mpito
huzingatia
mkakati na mbinu za utekelezaji wa sera hizo ili kufikia lengo.
Historia inadhihirisha kuwa CCM kimekuwa kikifanya mambo hayo kwa
kuzingatia Kanuni ya wakati na mahali na ndiyo maana wananchi
wameendelea
kuwa na imani na Chama hicho na hivyo kuendelea kukipa ridhaa ya
kuongoza
nchi.
Umuhimu wa kanuni ya wakati na mahali katika ujenzi wa Ujamaa na
Kujitegemea umezingatiwa na nchi zote zinazojenga Ujamaa duniani
kote.
China kwa mfano, inajenga Ujamaa kwa kuzingatia historia, mazingira
na
hali halisi ya China katika dunia ya utandawazi. Hivi sasa China
inajenga
Ujamaa kwa kutekeleza mageuzi ya kiuchumi na kufungua milango hivyo
kukaribisha wawekezaji na kutoa kipaumbele kwa ushiriki wa sekta
binafsi,
tofauti na uchumi hodhi chini ya dola kama ilivyokuwa hapo awali.
Tanzania sio kisiwa katika dunia. Leo hii dunia nzima inatumia sekta
binafsi na kuwaingiza wananchi katika mfumo mzima wa kiuchumi.
Hapa Tanzania katika kujenga Ujamaa na Kujitegemea, Chama cha
Mapinduzi
wakati wote kinazingatia mawazo ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu
Julius K.
Nyerere kuhusu kutumia kanuni ya wakati na mahali kama alivyoainisha
katika kitabu chake cha UJAMAA (rejea Hotuba aliyotoa Chuo Kikuu cha
Cairo, tarehe 10 April 1967). Kabla ya Mwalimu kufariki dunia,
alisafiri
nchi mbalimbali duniani na mara ya mwisho alikwenda Ujerumani na
kushawishi wafanyabiashara waje kuwekeza nchini Tanzania na
alichofanya
Rais Jakaya Kikwete ni kuwashawishi wawekezaji toka nchi mbalimbali
na
ndani ya nchi waje kuwekeza nchini mwetu na kushamirisha uchumi ili
kupata
nguvu ya kuweza kufikia lengo kwa kuwashirikisha na kwa hiyo
kuwaingiza
wananchi katika mfumo mzima wa kukuza uchumi.
Hulka hii ya kwenda na wakati ndiyo iliyowapa imani Watanzania na
hivyo
kukichagua Chama Cha Mapinduzi kwa kishindo katika chaguzi
mbalimbali.
Kwa hiyo basi mawazo yaliyomo katika Gazeti la Tanzania Daima la
tarehe
28/1/2007 – ISSN 0856-9762 Toleo Na. 786 yametolewa bila kuzingatia
uhalisi wa historia, hali halisi ndani ya CCM na Serikali na bila
kufanya
uchambuzi wa kutosha.
Aidha, kwa Chama chochote makini kama kilivyo Chama cha Mapinduzi ni
vigumu kutenganisha fikra za kiongozi mkuu wa Chama na Chama chake.
Aliyoyasema Rais Jakaya Kikwete ambaye ndiye Kiongozi Mkuu na
Msemaji Mkuu
wa Chama ndiyo msimamo wa Chama ambao chimbuko lake ni Katiba ya
Chama na
Sera za Msingi za CCM.
Katika kutambua hilo Ilani ya CCM ya mwaka 2005 imejiwekea majukumu
mawili
ya msingi.
- Kuitoa Tanzania kutoka kwenye dimbwi la uchumi ulionyuma na
tegemezi na
kuiingiza katika mkondo wa uchumi wa kisasa wa Taifa linalojitegemea.
- Kuwashirikisha wananchi wote kwa njia ya uwezeshaji katika ujenzi
wa
uchumi na kuutokomeza umaskini.
Katika kutekeleza majukumu haya mawili ya msingi, Chama kimeainisha
mkakati wa kuwashirikisha wakulima na wafanyakazi katika mpango wa
Kukuza
Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania (MKUKUTA), Mkakati wa
Kurasimisha
Raslimali na Biashara Tanzania (MKURABITA) na mkakati wa Uanzishaji
wa
Maeneo Maalumu ya Uchumi (The Special Economic Zones Strategy).
Katika
kutekeleza MKUKUTA, kwa kuanzia Serikali imeshatoa shilingi bilioni
moja
kwa kila mkoa. Walengwa ni wakulima, wafanyakazi na wafanyabiashara.
Hali halisi inaonyesha uko mwingiliano mkubwa kati ya wakulima,
wafanyabiashara na wafanyakazi kiasi kwamba sio rahisi
kuwatenganisha
wakati wa kupanga mkakati wa maendeleo ya nchi. Wakulima kuna wakati
wanakuwa wakulima wa kujikimu aidha wakulima wafanyabiashara wa
mazao,
hii ni pamoja na wafugaji na wavuvi.
Wakulima wanatakiwa kubadilisha kilimo ili kitoe mchango wa uhakika
katika
ukuaji wa uchumi kwa kuanzisha kilimo cha kibiashara kwa mkulima
mmoja
mmoja au kwa ushirika. Kwa hiyo mtazamo na mwelekeo wa CCM ni
kuwafanya
wakulima walime kibiashara. Na kwa mantiki hiyo hata wafugaji na
wavuvi.
Katika hali hiyo kusema CCM kimewasahau wakulima na wafanyakazi siyo
sahihi. Hili wananchi wanalitambua vema na limedhihirishwa kama
ilivyoelezwa awali, na ridhaa ya asilimia zaidi ya 80 ya kura
alizopewa
Rais Jakaya Kikwete katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.
Rais Jakaya Kikwete kwa jinsi anavyokifahamu Chama chake, na
wanaokiunda,
kamwe hawezi kuwakana wakulima na wafanyakazi wa nchi hii kwa
gharama
yoyote ile.
Kwa hiyo CCM kinataka wananchi waelewe kuwa anachosisitiza Rais ni
kuwafanya Watanzania washiriki katika kujenga uchumi wa kisasa
katika
mazingira ya kisasa ya kubadilisha kilimo ili kiwe kilimo cha
kibiashara
na kwamba wafanyakazi waweze kujiajiri katika maeneo mbalimbali
ambayo
yameainishwa katika Ilani.
Hotuba ya Rais ni sehemu ya mchakato wa kuwafanya wananchi waelewe
na
hatimaye washiriki katika majukumu hayo. Alichozungumza kuhusu
nafasi ya
wafanyabiashara katika kuleta mapinduzi ya kilimo kutokana na uwezo
wao,
ni dalili ya kutosha kuthibitisha jinsi Rais anavyotambua
muingiliano kati
ya sekta ya kilimo na biashara. Aidha, inaonyesha jinsi anavyotaka
hali ya
wakulima iwe bora zaidi.
Ni matumaini ya Chama cha Mapinduzi kwamba Umma utakuwa umetuelewa,
na
kwamba wale wanaojaribu kupotosha kwa malengo yao wenyewe wataacha
kufanya
hivyo.
Ni matumaini yetu pia, kwamba hata wale wenzetu wenye alama za jogoo,
ngumi vidole, mizani n.k. katika bendera zao nao watakuwa wamejua
kwamba
alama ya nyundo na jembe zinawakilisha makundi mbalimbali katika
Chama Cha
Mapinduzi wakiwemo wakulima, wafanyakazi na wafanyabiashara ambao
ndio
tegemeo kubwa la Watanzania katika kujenga uchumi wa kisasa na wa
Taifa
linalojitegemea.
|