HISTORIA YA CCM TANGU TANU NA ASP

 

 

1.0     UTANGULIZI:

 

1.1            Maelezo ya awali

 

Chama cha Mapinduzi (CCM) kilizaliwa tarehe 5 Februari, 1977 kutokana na kuvunjwa  kwa vyama vya Tanganyika African National Union (TANU) na Afro-Shirazi Party (ASP). 

 

Tendo hilo la kihistoria lilikuwa ni la kuendeleza utamaduni uliokuwa umeanza huko nyuma wa kuunganisha nguvu kwa lengo la kujiimarisha katika mapambano.  Kwa mfano, ASP kwa upande wa Zanzibar ilitokana na kuungana kwa African Association (AA) na Shirazi Association (SA), tendo ambalo liliunganisha nguvu za wanyonge katika mapambano ya kuundoa usultani na utawala wa kikoloni wa Kiingereza.  Kwa upande wa Tanzania Bara, TANU ilitokana na kujibadilisha kwa Tanganyika African Association (TAA) kutoka jumuiya ya kutetea maslahi ya kijamii na kuwa chama cha siasa.

 

Kupatikana kwa uhuru wa Tanganyika tarehe 9 Desemba, 1961 na ule wa Zanzibar kupitia Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964, kulifanya TANU na ASP viwe vimekamilisha jukumu la ukombozi wa nchi hizi kutoka makucha ya ukoloni mkongwe na usultani.  Hata hivyo, vyama vya siasa hivi viliendelea kukabiliwa na majukumu ya kuendeleza mapambano ya ukombozi katika Afrika  na kote duniani; kujenga Tanganyika na Zanzibar huru kiuchumi na kijamii na kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa,

 

Katika mazingira ya ubeberu duniani wakati huo na hali ya unyonge wa mataifa haya machanga, yakielewa kuwa ‘umoja ni nguvu’, Tanganyika na Zanzibar zilibaini umuhimu wa muungano, hivyo ziliamua kuungana tarehe 26 Aprili, 1964.  Muungano huo ndio uliowezesha kuzaliwa kwa Tanzania.  Chini ya Muungano huo, Tanzania iliendelea kuwa na vyama vya siasa viwili, yaani TANU na ASP katika mazingira ya chama kimoja cha siasa.  Vyama hivi vilitambua fika kwamba vinahitaji chombo madhubuti cha uongozi katika kutekeleza majukumu yake ya ukombozi kwa ukamilifu hivyo uamuzi ulifanywa rasmi wa kuvunja TANU na ASP na kuundwa kwa Chama Cha Mapinduzi tarehe 5 Februari, 1977.

 

Katiba ya CCM, katika Azimio la Mkutano Mkuu wa Taifa wa Pamoja wa TANU na ASP tarehe 21 January, 1977, inaeleza kuwa, (uk. 2-3), “...kwa kauli moja tunaamua na kutamka rasmi kuvunjwa kwa Tanganyika African Union(TANU) na Afro-Shirazi Party (ASP) ifikapo tarehe 5 Februari, 1977 na wakati huohuo kuundwa kwa Chama kipya cha pekee na chenye uwezo wa mwisho katika mambo yote kwa mujibu wa Katiba.”

 

Muungano wa TANU na ASP ndio uliowezesha CCM kuwa Chama chenye  nguvu, imara na madhubuti, hivyo kuwa Chama cha siasa pekee chenye uwezo wa hali ya juu wa kuwaunganisha Watanzania. Aidha, CCM kimeweza kuwaongoza wananchi katika mapambano ya kitaifa ya kiuchumi, kisiasa na kijamii kufuatana na mabadiliko mbalimbali yanayojitokeza ndani na nje ya nchi.CCM kimeendelea kupewa dhamana na wananchi ya kuunda serikali na kukamata dola tangu 1977 chini ya mfumo wa demokrasia ya chama kimoja  hadi sasa katika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, kufuatia mageuzi yaliyoidhinishwa na marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Tanzania Juni 1992.

 

1.2     Umuhimu wa kuielewa historia ya CCM na Vyama  vilivyokitangulia

 

Historia ya CCM tangu TANU na ASP ina umuhimu wa pekee katika Taifa letu katika kuelewa tulikotoka, tulipo hivi sasa na tunakoelekea.  Historia ya nchi yetu haiwezi kukamilika bila ya historia ya vyama hivi vya ukombozi.  Historia hutoa mafunzo na ni mwelekezaji pia, kwa hiyo ni wajibu wa Watanzania, hasa wanachama wa CCM kujifunza kutokana na historia yetu.  Kazi kubwa na ya msingi inayofanyika katika kujifunza historia hiyo, ni kurithisha  dhamira ya kujituma na kudumisha uhuru wa nchi yetu. Hivyo, ili kuendelea kukijenga Chama, na kuimarisha uwezo wa kuendelea kukamata dola barabara kwa namna endelevu, hapana budi ihakikishwe kuwa historia ya CCM inabeba pia jukumu la msingi la kusaidia:-

 

·        Kujua Chama kilikotoka, mahali kilipo na kinakoelekea katika misingi ya sera, itikadi, malengo na wanachama.

·        Kuunganisha wanachama na kuwaweka pamoja kiimani, kiitikadi na kiutendaji.

·        Wanachama kujitambua, kutambua wajibu na majukumu yao na kujenga moyo wa kujiamini na kujithamini.

·        Kuinua kiwango cha ushiriki wa wanachama wa CCM na wananchi katika kubuni na kutekeleza mkakati na mbinu sahihi za kutetea na kuendeleza Chama na taifa kufuatana na hali ya wakati na mahali.

·        Kuweka misingi ya kufanya tathmini na hivyo kuwa na uhakika katika kufanya maamuzi.

·        Kupanda mbegu bora za upendo, uzalendo na uchungu wa kweli kwa uhai wa CCM na taifa kwa ujumla.

·        Kuwa na majibu sahihi wakati wote kwa hoja mbalimbali zinazotolewa kuhusu Chama Cha Mapinduzi na taifa kwa ujumla.

·        Kuweka msingi wa kurithisha kutoka kizazi kimoja hadi kingine maadili ya msingi wa uhai wa CCM.

·        Kuhifadhi kuweka na kueneza kumbukumbu sahihi ya historia ya Chama, nchi, mchango wa Waasisi na wanachama na kuhakikisha wapotoshaji hawapati fursa ya kueneza uongo.

 

1.3     Chimbuko la Historia ya CCM

 

Pamoja na kwamba Chama Cha Mapinduzi kuwa kilizaliwa rasmi tarehe 5 Februari, 1977, chimbuko lake linaanzia miaka mingi kabla, sambamba na historia ya uhai wa taifa la Tanzania. Mizizi ya historia ya CCM imo ndani ya harakati za kukataa ukoloni na usultani, zilizofanywa na wananchi wa Tanzania. Wahenga wetu  kwa pamoja tangu enzi, walionyesha wazi kukataa kwao kutawaliwa. Historia ya Tanzania inao utajiri wa mifano mingi ya harakati hizo japokuwa zilijengwa katika misingi ya ukoo na ujirani, katika wilaya na mikoa mbalimbali hata kabla ya kuundwa kwa vyama vya TANU na ASP.

 

Wananchi hao waliotutangulia walikataa kunyonywa, kupuuzwa, kubaguliwa, kutawaliwa, kunyanyaswa na kugawanywa katika misingi ya rangi, kabila, dini, jinsia, nk. Utu na uhuru wao ulikuwa na thamani kubwa sana. Hivyo waliamua kupambana dhidi ya udhalimu huo. Baadhi ya mifano ya jitihada za mapambano ya awali ni Vita ya Majimaji huko Umatumbi na maeneo ya kusini, Mbiru huko Upare, Waluguru, Wameru, Wahehe na mengineyo huko Unguja, Pemba, Kanda ya Ziwa na katika jamii za wafugaji. Ari, utashi, uzalendo na dhamira ya kweli ya kutaka kujitawala vilivyojidhihirisha katika harakati hizo, viliotesha mizizi iliyoshikilia uhai wa vyama vya TANU na ASP.

 

2.0     TANU NA HARAKATI ZA KUPIGANIA UHURU WA TANGANYIKA

 

2.1     TANU ilizaliwa katika mazingira yaliyoandaliwa na Tanganyika African Association (TAA):

 

TAA iliundwa 1948 kufuatia tukio la kutengana kwa African Association (AA) ya Tanganyika na Zanzibar.  AA  ilizaliwa Dar es Salaam 1927 chini ya uongozi wa Cecil Matola akiwa Rais na Kleist  P. Sykes akiwa Katibu.  Malengo ya AA yalikuwa ni kupigania haki, maslahi na umoja wa Waafrika.  AA ilikuwa na matawi yake makuu Dodoma na Zanzibar.  Aidha, AA ilifungua matawi katika miji iliyokuwa makao makuu ya wilaya.

 

Katiba ya TAA ilitamka wazi kwamba Chama hicho hakikuwa na malengo ya kisiasa.  Mwaka 1953 yalifanyika mabadiliko ya uongozi katika TAA.  Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alichaguliwa kuwa Rais wa TAA.  Chini ya uongozi mpya, Katiba ya TAA ilionekana kwamba  isingeweza kukidhi malengo ya kisiasa.  Mwalimu alipewa jukumu la kuandaa Katiba mpya ya TAA ambayo ingezingatia malengo ya kisiasa.  Baada ya uandaaji wa Katiba hiyo kukamilika, haja ya kubadili jina ilionekana dhahiri na majina mengi yalipendekezwa likiwemo la TANU.  Nafasi ya TAA ilichukuliwa na TANU iliyozaliwa tarehe 7 Julai, 1954.  TANU  ilirithi matawi ya TAA, wanachama na viongozi wa TAA katika maeneo mengi.

 

Waasisi wa TANU ambao walihudhuria na kushiriki katika Mkutano wa kuzaliwa kwa TANU walikuwa 17:

 

(1)              Mwalimu J.K. Nyerere – Rais wa TAA/TANU

(2)              Geremano Pacha – Jimbo la Magharibi

(3)              Joseph Kimalando – Jimbo la Kaskazini

(4)              Japhet Kirilo – Jimbo la Kaskazini

(5)              C.O. Milinga – Jimbo la Mashariki

(6)              Abubakari llanga – Jimbo la Ziwa

(7)              L.B. Makaranga – Jimbo la Ziwa

(8)              Saadani A. Kandoro – Jimbo la Ziwa

(9)              Suleman M. Kitwara – Jimbo la Ziwa

(10)         Kisung’uta Gabara – Jimbo la Ziwa

(11)         Tewa Said Tewa – Jimbo la Mashariki

(12)         Dossa A. Aziz – Jimbo la Mashariki

(13)         Abdu Sykes – Jimbo la Mashariki

(14)         Patrick Kunambi – Jimbo la Mashariki

(15)         Joseph K. Bantu – Jimbo la Mashariki

(16)         Ally Sykes – Jimbo la Mashariki

(17)         John Rupia – Jimbo la Mashariki

 

2.2  TANU ilizaliwa baada ya Vita ya Pili ya Dunia:

 

Katika vita ya Pili ya Dunia (1939 – 1945), Watanganyika walishiriki wakiwa askari upande wa Waingereza.  Katika kushiriki huko, baadhi yao walipigana vita nchi za nje, kwa mfano, India, Burma, Madagascar n.k.  Wakiwa huko vitani walipata fursa ya kubadilishana mawazo ya kisiasa na askari wenzao waliokutana nao katika uwanja wa vita.

 

Baadhi ya askari hao wa Tanganyika waliporejea kutoka vitani walikuja na fikra mpya za ukombozi wa Mwafrika.  Fikra hizi mpya zilioana na zile za Kituo cha Wasomi wa Kiafrika waliokuwa  London.  Kituo hicho kilijishughulisha sana na suala la ukombozi wa Mwafrika kupitia midahalo.

 

2.3            TANU ilizaliwa katika mazingira  ya vyama vya ushirika:

 

Katika miaka 1950, wakulima walikwishajiunga na kuanzisha vyama vya kuuza mazao yao ya biashara ili waweze kupata bei nzuri kwa kupunguza gharama ya mtu wa kati ambaye alikuwa ni mfanyabiashara wa Kiasia.  Baadhi ya Vyama  vya Ushirika vilivyokuwepo kabla ya TANU ni:-

 

·                    Kilimanjaro Co-operative Union Ltd (1933)

·                    Ngoni – Matengo Co-operative Union Ltd. (1936)

·                    Rungwe African Co-operative Union Ltd. (1949)

·                    Bukoba Co-operative Union Ltd. (1950)

·                    Lake Province Native Growers Association.

 

Kwa kuwepo vyama vya ushirika, ujumbe wa TANU kuwafikia wananchi ulirahisishwa.  Wanachama wa vyama vya ushirika walijiunga na TANU.  Wanachama na viongozi wa vyama vya ushirika waliunga mkono TANU katika madai yake ya kudai uhuru.  Baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika walichaguliwa kuwa viongozi wa TANU katika ngazi ya Taifa.  Kwa mfano:-

 

·                    Ndugu Nsilo Swai

·                    Sir George Kahama

·                    Ndugu Jeremiah Kasambala

·                    Balozi Paul Bomani

·                    Ndugu John Mhavile.

 

TANU nayo iliunga mkono vyama vya ushirika katika madai yake ya bei nzuri ya mazao yao na kuondoa ushuru wa kahawa uliokuwa unatozwa na Serikali Kuu.  Aidha, TANU  ilihimiza na kuwahamasisha wananchi kuanzisha na kuimarisha vyama vya ushirika.  Kazi hii  ya kuhimiza na kuhamasisha wananchi kujiunga na ushirika iliendelea kufanywa na TANU hata baada ya Tanganyika kupata uhuru wake.

 

Baada ya Uhuru, TANU iliuona ushirika kuwa ni chombo cha kuleta maendeleo hivyo wananchi walihimizwa kuanzisha ushirika katika maeneo ambayo hayakuwa na vyama vya ushirika.  Hali hii inaendelea hadi hivi sasa ambapo katika mfumo wa uchumi wa Soko, CCM inauona ushirika kuwa ni chombo cha kumwezesha mwananchi kiuchumi katika kumiliki na kuendesha uchumi wa Taifa lake.

 

2.4  TANU ilizaliwa katika mazingira ya  vyama vya wafanyakazi:

 

Lengo kuu la Vyama vya Wafanyakazi lilikuwa ni kutetea maslahi ya wafanyakazi.  Baadhi ya vyama vya wafanyakazi ni:-

 

·                    Chama cha Wafanyakazi Serikalini (1929)

·                    Chama cha Makuli (1937)

·                    Chama cha Wapishi na Madobi (1939)

·                    Chama cha Wapishi na Watumishi wa Ndani

·                    Chama cha Madereva

·                    Chama cha Walimu

·                    Chama cha Wafanyakazi wa Reli

·                    Chama cha Wafanyakazi Mashambani

·                    Chama cha Wafanyakazi Viwandani.

 

Vyama vya Wafanyakazi viliunda Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tanganyika Federation  of Labour –TFL) tarehe 10 Oktoba, 1955.

 

Wafanyakazi kupitia vyama vyao walikuwa na madai yafuatayo:-

 

·                    nyongeza ya mshahara

·                    mapumziko ya mchana siku ya kazi

·                    umri wa kustaafu na

·                    kuondoa ubaguzi katika ajira na huduma za jamii.

 

Vyama vya wafayakazi vilisaidia kuvunja ukabila na hivyo kuwa chanzo cha umoja.  Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi lilisaidia kueneza TANU kwa njia zifuatazo:-

 

·                    Kila Chama cha Wafanyakazi chini ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TFL) kilitakiwa kuwashawishi na kuwahimiza wanachama wake kujiunga na TANU.

·                    Kila mwanachama wa TANU aliyekuwa mwanachama wa Chama cha Wafanyakazi alitakiwa kulipa mchango wake wa kila mwezi kwa TANU.

·                    Vyama vya Wafanyakazi, wakati mwingine kupitia TFL, viliweza kusaidia TANU kifedha fedha hizo zilitokana na michango ya hiari.

·                    Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi lilisaidia sana kuleta mwamko wa kisiasa miongoni mwa wafanyakazi.

 

Vyama vya Wafanyakazi vilifanya yote hayo kwa kuelewa kwamba uhuru ndio ungekuwa suluhisho la kweli la matatizo yao.

 

Kama ilivyokuwa kwa vyama vya ushirika, baadhi ya viongozi wa vyama vya wafanyakazi walichaguliwa kuwa viongozi wa TANU.  Mwaka 1958, Katibu  Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi, Mzee Rashid Mfaume Kawawa, alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya TANU.  Toka wakati huo hadi hivi sasa, Mzee Kawawa amekuwa  na uongozi uliotukuka katika TANU/CCM.

 

Kwa upande wake, TANU iliunga mkono madai ya vyama vya wafanyakazi na migomo ya wafanyakazi.  Katika historia ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi, mgomo wa wafanyakazi wa Shamba la Mazinde huko Tanga na mgomo wa wafanyakazi wa Kiwanda cha Bia Dar es Salaam ni miongoni mwa migomo maarufu.

 

Shamba la Mazinde lilikuwa mali ya bepari mmoja wa Kiingereza, mwanachama mashuhuri wa United Tanganyika Party (UTP) aliyewahi kushiriki katika kugombea na kushindwa na mgombea wa TANU katika Uchaguzi Mkuu wa Baraza la Kutunga Sheria mwaka 1958.  Wafanyakazi katika Shamba la Mazinde walijiunga na Chama cha Wafanyakazi Mashambani (Tanganyika Plantation Workers’ Union – TPWU) ambacho kilikuwa kimeshirikishwa katika Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi.  Mmiliki wa Shamba la Mazinde alikuwa na tabia ya kuwafukuza wafanyakazi walioonyesha kupinga UTP na walioamua kujiunga na Chama cha Wafanyakazi Mashambani.  Katika harakati za kuwaunga mkono wenzao waliofukuzwa, wafanyakazi wote elfu tatu (3,000) waliamua kugoma na matokeo yake wote walifukuzwa kazi.

 

Jitihada za TFL kusuluhisha mgogoro huo kati ya Mwajiri na wafanyakazi zilishindikana.  TFL na TANU kwa pamoja viliunga mkono mgomo wa wafanyakazi wa Shamba la Mazinde.  TANU kupitia Mwalimu Nyerere ilitoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Tanga kuwahifadhi  wafanyakazi waliofukuzwa kazi.  Wananchi waliitikia wito wa TANU na kuwapokea na kuishi nao.  Aidha, TFL na TANU vilitoa wito kwa wananchi kususia shamba la Mazinde.  Wafanyakazi hao hawakurejea kazini hata baada ya mmiliki kuwataka kufanya hivyo.  Matokeo yake ni kwamba mmiliki huyu wa Shamba la Mazinde hakuchukua muda akafilisika na akarejea kwao Uingereza.

 

Huu ulikuwa ni ushindi wa TANU na TFL.  TANU ilitambuliwa na wafanyakazi mashambani na iliendelea kuimarika.  Kwa kuwa ngome ya UTP, na baadaye African National Congress (ANC) ilikuwa huko Tanga  pigo hili lilisababisha kifo cha UTP na kuzorota kwa ANC.

 

Kuhusu mgomo wa Kiwanda cha Bia Dar es Salaam, mgomo ulianza Aprili hadi Juni, 1958.  Mgomo uliwashirikisha wafanyakazi wapatao  mia tatu (300).  Wafanyakazi walikuwa wanadai nyongeza ya mshahara.  Wafanyakazi wote waliogoma walifukuzwa kazi na mwajiri.

 

Katika kuonyesha mshikamano na wafanyakazi katika mgomo huu wa Kiwanda cha Bia, TANU ilichukua hatua zifuatazo:-

 

·                    Ilitoa wito kwa nchi nzima kususia pombe zote za kigeni;

·                    Iliwaomba wananchi wa Dar es Salaam kuwasaidia wagomaji kwa kuwachangia chakula na fedha;

·                    Iliwaomba wananchi wenye nyumba Ilala kuwapokea wagomaji katika nyumba zao pasipo kuwatoza kodi ya nyumba.

 

Kama kawaida yao, wananchi waliitika wito na maombi ya TANU.  Kwa kupitia migomo  TANU ilizidi kuimarika miongoni mwa wafanyakazi.

 

2.5     TANU ilizaliwa katika mazingira ya kero na adha za wananchi kutoka  Serikali ya Kikoloni:                                          

           

Malalamiko hayo ya wananchi yalijidhihirisha katika maeneo yafuatayo:-

 

·                    Upinzani huko Upare dhidi ya ulipaji kodi kulingana na  mapato (Mbiru);

·                    Wahehe kukataa kuogesha ng’ombe wao;

·                    Waluguru kupinga juhudi za kuhifadhi mapori na kulima matuta;

·                    Wafugaji (Wasukuma) kupinga kodi ya ng’ombe na kupunguza idadi ya ng’ombe, kumi kwa kila mia;

·                    Wameru wapatao 3,000  walipinga  kunyang’anywa ardhi yao na Serikali ya Kikoloni na kuwapa walowezi.

 

TANU ilitumia kero hizo za wananchi katika kuwaunganisha wananchi na kuwaelekeza namna ya kutafuta haki zao.

 

Kuhusu ardhi ya Wameru, Katika mkutano wake wa kwanza, TANU ilitoa tamko lifuatalo:-

 

“Mkutano huu unasikitika sana juu ya mambo yaliyofanywa na Serikali ya nchi hii huko Meru.  Mkutano unakubali kwamba Serikali inayo mamlaka kuchukua ardhi ya raia hata kwa lazima ili ardhi hiyo iwe faida ya watu wote kama vile kupitisha reli, barabara, kujenga hospitali, shule au kutumia kwa jambo lingine la manufaa kwa wote.  Lakini Serikali haina mamlaka kuchukua ardhi ya raia ili ardhi ile wapewe raia  wengine waitumie kwa faida yao wenyewe   Mkutano huu unataka Serikali iwarudishie Wameru ardhi  yao ama kuwalipa fidia kwa hasara walizopata kubwa, kwa kufukuzwa kama mahabusu, kama Baraza la Umoja wa Mataifa lilivyokubaliana.”  (Historia ya Chama cha TANU 1954 hadi 1977, uk 36).

 

 

2.6      Kuenea kwa TANU na Kupata Ushindi:

 

Dhumuni la kwanza la TANU mwaka 1954 lilikuwa ni kuwatayarisha Watanganyika kujitawala na kujitahidi  kwa bidii mpaka Tanganyika imepata uhuru na inajitawala.  TANU ilibaini kwamba lengo lake kuu ni kupigania uhuru wa Tanganyika na silaha yake kubwa ni umoja hasa umoja wa Waafrika.  Kwa mnasaba huo, TANU iliacha mlango wake wazi kwa Waafrika bila ya kujali kabila, dini, rangi, jinsia  na majimbo yao.  Toka mwanzo, msingi huu uliifanya TANU kuwa chama cha umma.  Hata hivyo uamuzi wa kukifanya Chama cha TANU kuwa wazi kwa Waafrika tu ulikuwa ni uamuzi wa kimkakati tu.  Haikukusudiwa kukifanya Chama hicho kuwa cha kibaguzi na  kwa hakika kiliendelea kushirikiana na kuwaenzi Waasia na Wazungu walioafiki imani na madhumuni ya TANU.Miongoni mwa Waasia na Wazungu waliokuwa na mtazamo wa kizalendo katika shughuli za kisiasa ni Amir Jamal, Al-Noor Kassim, Derek Bryceson, Babra Johnson na Leader Stirling.  Baada ya uhuru (1962), Waasia na Wazungu waliruhusiwa kuwa wanachama wa TANU.

 

Katika harakati za kuitangaza TANU, njia mbali mbali zilitumika:-

 

·                    TANU ilifungua matawi katika maeneo mbali mbali ya nchi yetu.

·                    TANU ilitumia mikutano ya hadhara katika kufikisha ujumbe wake kwa wananchi.

·                    TANU ilitumia mikutano ya ndani ya wanachama.

·                    TANU ilitumia vyombo vya habari, hususan magazeti, kama vile Sauti ya TANU, Habari za TANU na Mwafrika.

 

2.7     Jumuiya za TANU za Umoja wa Wanawake, Umoja wa Vijana na Wazazi zilifanya kazi kubwa katika kukieneza na kukiimarisha Chama.

 

TANU ilianzisha rasmi mwaka 1955 sehemu ya Wanawake wa TANU.  Chama kilitambua kwamba mapambano ya kudai uhuru yasingeweza kufanikiwa bila ya kulitumia jeshi kubwa la Wanawake.  Chama kilimpata Bibi Titi Mohamed na kumpa jukumu la kuwakusanya wanawake ili washiriki katika mapambano ya kudai uhuru.  Sehemu ya Wanawake ilipewa majukumu yafuatayo:-

 

·                    Kupata wanachama wa TANU wengi;

·                    Kueneza Chama hasa vijijini kwa moyo wa kujitolea;

·                    Kuona kwamba viongozi wa Chama wako salama/ulinzi wa viongozi  na

·                    Kukipatia Chama fedha  kutokana na shughuli halali  mbali mbali.

 

Katiba ya TANU ya mwaka 1954, sehemu ya sita, ilitoa nafasi kwa vijana kuunda umoja wao ili waweze kushiriki kwa ukamilifu katika mapambano ya kudai uhuru.  Umoja wa Vijana ulikuwa na majukumu yafuatayo:

 

·                    Kuwaandaa vijana katika uongozi;

·                    Kuwahimiza vijana kujitolea kufanya kazi za TANU;

·                    Kutekeleza shabaha za TANU;

·                    Kuunda makundi ya starehe na maendeleo miongoni mwa wanachama kama vile, elimu, biashara na michezo;

·                    Kukusanya habari na kufuatilia mwenendo wa kisiasa nchini;

·                    Kushirikiana na vyama vingine vya vijana visivyo na upinzani kwa TANU.

 

2.8     TANU ilivyopambana na kuvishinda vikwazo na hila za Mkoloni

 

Jumuiya ya Wazazi (Tanganyika Parent’s Association – TAPA) iliundwa mwaka 1955 chini ya Ndugu Lawi Sijaona. TAPA ilikuwa ndiye mtekelezaji mkuu wa Azimio la Mkutano Mkuu wa Tabora lililohusu upanuzi wa elimu.  Katika kutekeleza jukumu lake, TAPA ilifungua shule za msingi na sekondari nyingi nchini na kuendesha kisomo cha Watu Wazima.  Huu ulikuwa mkakati wa makusudi wa kuwaandaa wananchi kushika madaraka baada ya uhuru.

 

Jinsi TANU ilivyozidi kuimarika ndivyo hivyo ilivyopambana na vikwazo na hila za Mkoloni:

 

·                    Serikali ya Kikoloni ilipitisha Sheria mwaka 1953 ya kuwakataza watumishi wa Serikali wa mataifa yote kujiunga na vyama vya siasa.  Aidha, Tangazo la Serikali Namba 2 la 1954 lilifafanua kuwa hata Sukuma Union kilikuwa ni Chama cha Siasa.  Kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Namba 6 la 1954, maafisa wote wa Serikali waliokuwa wanachama wa TANU na waliotaka kuendelea na utumishi serikalini walitakiwa kujiuzulu mara moja.  Aidha, Sheria ya vyama vya siasa, 1954, ilitaka kila tawi la TANU lisajiliwe kabla ya kuandikishwa kisheria.  Sheria hii iliiwezesha serikali ya mkoloni kusajili au kutokusajili tawi lo lote la TANU.

 

·                    Mara tu baada ya TANU kuundwa, Rais wake Mwalimu Nyerere alitakiwa na Serikali ya Kikoloni achague moja kati ya mambo mawili ama kuendelea kuiongoza TANU au kujiuzulu  uongozi wa TANU na kuendelea na kazi yake ya ualimu katika Shule ya Sekondari Pugu.   Mwalimu aliamua kuendelea  kuihudumia TANU hivyo akalazimika kujiuzulu kazi ya ualimu.  Bila shaka, Serikali ya Kikoloni ilidhani kwamba Mwalimu asingejiuzulu ualimu.  Katika suala hili, uamuzi wa Mwalimu haukuwa rahisi hasa kwa kuzingatia kwamba kazi ya ualimu ndio alikuwa ameisomea, riziki yake na ya familia ilitokana na ualimu na kwamba kuitumikia TANU wakati huo ilikuwa ni kupambana na Serikali ya Kikoloni na hii ilikuwa ni hatari kubwa.  Kwa kujiuzulu ualimu, Mwalimu alipata nafasi kubwa zaidi ya kuihudumia TANU.

 

·                    Mwalimu Nyerere mwaka 1958 alishitakiwa na Serikali ya Kikoloni kwa kosa la kuwakashifu District  Commissioners wa Songea, Geita na Musoma.  Kwamba kashfa hiyo aliifanya kwa kupitia makala aliyoiandika kupitia Gazeti la “Sauti ya TANU” Toleo Namba 29 la tarehe 27 Mei, 1958.   Katika kesi hii iliyosikilizwa na Mahakama ya Dar  es Salaam, Mwalimu  alihukumiwa faini ya shs. 3,000/= (shilingi elfu tatu) au kifungo cha miezi 6.  Mwalimu alilipiwa faini hiyo na TANU.

 

·                    Serikali ya kikoloni pia ilijitahidi kadri ilivyoweza kuwatumia baadhi ya machifu  kuwa chombo cha kuzuia uenezaji wa TANU.  Machifu walipewa madaraka makubwa zaidi na zaidi ili wajisikie kuwa ni sehemu ya utawala na kwamba TANU ilikuwa na lengo la kuwakosesha maslahi yao.  Mwaka 1957, Serikali ya kikoloni iliunda Baraza la Machifu wa Tanganyika (Territorial Convention of Chiefs).  Kwa kuwatumia machifu, Serikali ya kikoloni ilitegemea kuwagawa Watanganyika kwa misingi  ya ukabila ili kuweza kuwatawala wananchi kwa urahisi zaidi.  Aidha, Serikali ya kikoloni ilikuwa na lengo la kuwagonganisha machifu na viongozi wa TANU.

 

·                    Serikali ya kikoloni ilihimiza kuundwa kwa United Tanganyika Party (UTP) ndani ya Baraza la Kutunga Sheria mwaka 1956.  UTP ilikuwa ni chombo na Sauti ya Serikali ya kikoloni kwa sababu zifuatazo:-

 

(a)              Uongozi wa UTP uliundwa na Wajumbe wa Baraza la Kutunga Sheria,

Tanganyika Unofficial Members Organization (TUMO)”

(b)              Wajumbe hao waliteuliwa na Gavana na hivyo hawangeweza kupingana na siasa ya Serikali ya Kikoloni.

 

Licha ya hila na vikwazo vya mkoloni, TANU ilijikuta ina mtihani mgumu wa kuamua kushiriki ama kutokushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa kwanza  mwaka 1958.  Akifungua kikao cha kwanza cha Baraza la Kutunga Sheria mwaka 1956, Gavana Edward Twining alitangaza kuwa Serikali ilikuwa na mpango wa kufanya Uchaguzi Mkuu wa kwanza mnamo 1958.  Sharti moja kubwa la uchaguzi huo lilikuwa kwamba kila mpiga kura apige kura tatu:  moja kwa Mzungu, moja kwa Mwasia na moja kwa Mwafrika.

 

Suala hili la kura ya Mseto lilijadiliwa kwa undani katika Mkutano Mkuu wa TANU uliofanyika Tabora mwaka 1958 na kuhudhuriwa na Wajumbe 300 kutoka sehemu zote za Tanzania Bara.  Ili kupata nafasi nzuri ya kujadili agenda hii, Mwalimu Nyerere aliomba asiwe Mwenyekiti wa kikao hicho, nafasi yake ilichukuliwa na Mwalimu Kihere kutoka Tanga.

 

Mwalimu Nyerere aliweza kuushawishi Mkutano kukubali kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa kwanza mwaka 1958.  Hoja za Mwalimu zilikuwa ni kwamba kama TANU isingeshiriki, ingekuwa imeshindwa kwani isingekuwa na wawakilishi katika Baraza la Kutunga Sheria.  Kujitoa katika uchaguzi huo kungekuwa na maana ya kujitoa katika uwanja wa mapambano ambao sasa ungemilikiwa na UTP.  Uamuzi wa TANU kushiriki katika uchaguzi huo ulikuwa ni wa busara kwani wagombea wote waliosimamishwa kwa tiketi ya TANU walishinda na hivyo TANU kunyakua viti vyote vya wajumbe wa kuchaguliwa wa Baraza la Kutunga Sheria.

 

Matokeo ya kukubali kura ya mseto, aliyekuwa Katibu Mwenezi wa TANU, Ndugu Zuberi Mtemvu aliamua kuachana na TANU na kuanzisha African National Congress (ANC) mwaka 1958.  Hata hivyo toka kuanzishwa kwake hadi kifo chake, ANC haikupata hata kiti kimoja katika Baraza la Kutunga Sheria.  Aidha, Ndugu Mtemvu alibwagwa kwa kishindo na Mwalimu Nyerere katika kugombea Urais wa Jamhuri ya Tanganyika mwaka 1962.

 

Uchaguzi Mkuu wa pili ulifanyika mwaka 1960.  Katika uchaguzi huo, TANU ilijikuta imefanikiwa kupitisha wagombea wake 58 bila ya kupingwa.  Kati ya wagombea hao 58 waliopita bila kupingwa, 8 walikuwa Wazungu, 11 Waasia na 39 Waafrika.  Tarehe 30 Agosti, 1960 ulifanyika uchaguzi katika sehemu nyingine ambako kulikuwa na zaidi ya mgombea   mmoja katika jimbo la uchaguzi.  Wagombea viti wote jumla walikuwa 25 kati ya hao 11 walisimamishwa na TANU na walishinda isipokuwa mmoja tu wa kiti cha Mbulu, Chifu Amri Dodo aliyeshindwa na Herman E. Sarwatt ambaye alikuwa mgombea binafsi.  Hata hivyo, Sarwatt alikuwa ni mwanachama wa TANU.

 

Pamoja na vikwazo hivi Msimamo sahihi usioyumba uongozi bora umoja mshikamano ari na dhamira ya wananchi ya kutaka kujitawala vilikuwa chachu iliyosababisha TANU kupata  ushindi wa kishindo na kutokana na ushindi huo, Gavana  Richard Turnbull alimwomba Rais wa TANU, Mwalimu Nyerere kuunda Baraza la Mawaziri ambalo lilikuwa na jukumu la kuongoza nchi kwa jumla na kumshauri Gavana.  Serikali ya Madaraka iliundwa na kuapishwa tarehe 3 Septemba, 1960.  Tanganyika ilipata Serikali ya Ndani  tarehe 1 Mei, 1961 na uhuru kamili tarehe 9 Desemba, 1961 na Mwalimu Nyerere kuwa Waziri Mkuu wa Kwanza wa Tanganyika huru.

 

2.9     Siri ya ushindi wa TANU

 

Uhuru wa Tanganyika ulipatikana katika kipindi cha miaka  saba tu ya kudai uhuru.  Kipindi hiki ni kifupi.  Siri ya TANU ya ushindi ilitokana pamoja na mambo yafuatayo:-

 

·                    Tanganyika  ilikuwa chini ya Udhamini wa Umoja wa Mataifa tofauti na nchi kama Kenya, Uganda, Zambia na Malawi zilizokuwa makoloni moja kwa moja chini ya Serikali ya Kiingereza iliyokuwa  na sauti ya mwisho.  Chini ya  udhamini huo  watawala wa Kiingereza, walipaswa kuitawala nchi hii kwa mujibu wa masharti ya Umoja wa Mataifa kuhusu makoloni ya udhamini.

 

·                    Nafasi ya Jamhuri ya Kisovieti (Urusi)  (ilikuwa miongoni mwa mataifa manne makubwa) katika Umoja wa Mataifa ilisaidia kutoa msukumo kwa Umoja huo katika kufanikisha juhudi za TANU za kudai uhuru wa Tanganyika.  Aidha, Urusi ilikuwa ni Mjumbe wa Baraza la Udhamini.  Msimamo wa Urusi kuhusu makoloni ulikuwa thabiti kwamba makoloni yana haki ya kujitawala. Uhuru wa India, Pakistani na Ghana ulisaidia kutoa msukumo kwa makoloni kujipatia uhuru.

 

·                    Lugha ya Kiswahili ilisaidia sana katika kuharakisha maendeleo ya siasa.  Kiswahili kilisaidia kuwaunganisha wananchi na hasa kilirahisisha kazi ya viongozi wa TANU.  Viongozi hao hawakuhitaji wakalimani wakati wa kuwahutubia wananchi katika mikutano ya hadhara.  Lugha  ya Kiswahili  ilisaidia na inaendelea kusaidia katika kuleta umoja na mshikamano wa kitaifa. 

 

·                    Katika Tanganyika hapakuwepo na mtengano  wa kijamii wenye nguvu.  Tanganyika ilikuwa na makabila yapatayo 120 lakini kihistoria hapakuwa  na utawala wa kikabila wa kugandamiza kabila lingine.

 

·                    Tanganyika ilikuwa na walowezi wachache ikilinganishwa na nchi kama Kenya.  Katika makoloni mengi uhuru wa wananchi ulicheleweshwa kutokana na siasa za walowezi ambazo msingi wake ni uchumi hodhi.

 

·                    Umoja wa Vijana na Umoja wa Wanawake chini ya TANU, walitoa  msukumo mkubwa katika kudai uhuru.  Vikundi hivyo vilijawa na ari na moyo wa kimapinduzi; vilifanya kazi ya kujitolea usiku na mchana.

 

·                    Vyama vya Wafanyakazi na Vyama vya Ushirika viliweza kuwabana vilivyo Wakoloni kwa njia ya migomo na ususiaji wa bidhaa.

 

·                    Uongozi bora wa TANU, hususan uongozi wa Mwalimu Nyerere.  Uongozi bora wa TANU ndio uliokipa Chama msimamo thabiti na kuwafanya wananchi kuwa na imani kubwa na TANU.

 

Aidha TANU iliweza kushinda changamoto katika sura ya hila na vikwazo kadhaa na kupata mafanikio kama vile:-

 

3.0     ASP   NA  HARAKATI ZA MAPAMBANO DHIDI YA  UKOLONI WA KIINGEREZA NA USULTANI WA KIARABU

 

3.1                      Mazingira ambamo ASP  ilizaliwa:

 

·                    ASP ilizaliwa katika mazingira yaliyokwisha andaliwa kisiasa na African Association (AA) na Shirazi Association (SA); vyama ambavyo vilikuwa nusu vya siasa na nusu vya kupigania maslahi ya Watumishi wa Kiafrika kazini.  Katika mazingira hayo, waafrika na Washirazi walielewa kwamba:-

 

(a)              Adui wa Waafrika ni ukoloni wa Kiingereza na umwinnyi wa Kiarabu ukiongozwa na Sultani.<