Chama Cha Mapinduzi

MADA:  CHAMA CHA MAPINDUZI NA SERIKALI    ZAKE WAFANYE NINI ILI KUFAIDIKA NA MFUMO WA UTANDAWAZI

Makala kwa ajili ya semina ya Wenyeviti na Makatibu wa CCM wa Mikoa na Wilaya

Prof. D.S. KAPINGA

24 AGOSTI, 2004

_______________________________________________________________________________

            Katika kipindi kati ya uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995 na sasa, mabadiliko yaliyotokea duniani ni kuiimarisha zaidi kwa dhana ya kuwa na dunia inayofuata   itikadi moja, siasa moja, uchumi na utamaduni mmoja ambamo dunia ni           kama kijiji” (Ilani ya Uchaguzi Mkuu, 2000, ibara ya 8, mkazo umeongezwa).

_____________________________________________________________________________________________________________

 1. UTANGULIZI

Nukuu hii kutoka Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2000 ina umuhimu wa     pekee katika mjadala kuhusu utandawazi na hasa maneno yaliyotiliwa mkazo. Utandawazi unaipa dunia sura inayofanana na mahusiano katika kijiji. Teknologia        ya habari na mawasiliano (teknohama) ndiyo hasa iliyoifanya dunia iwe kama kijiji.

Katika kitabu: Jubilei ya Miaka Ishirini na Tano ya Chama cha Mapinduzi,         1977 – 2002, tunasoma:

“Uundaji wa mazingira ya uchumi wa soko huru unafanyika katika mazingira ya utandawazi ambao sifa yake kubwa ni ushindani katika soko la dunia ambayo kutokana na mapinduzi katika teknolojia ya upashanaji habari (Information and Communication Technology – ICT) imekuwa kama kijiji. Hivi sasa, wazalishaji, walaji na wadau wengine waliotenganishwa kijiografia na makontinenti wanaweza kuwasiliana  katika         dakika chache bila kuonana” (uk. 3).

Umuhimu mwingine wa nukuu kutoka Ilani ni hii dhana ya utandawazi kama    jitihada ya nchi za magharibi kuwa na dunia         inayofuata itikadi moja, siasa moja,      uchumi na utamaduni mmoja, dhana ambayo mara nyingi haijitokezi katika    mijadala kuhusu utandawazi. Soko huru linalozungumzwa kuhusu utandawazi   siyo la fedha na bidhaa tu, bali pia siasa, itikadi, utamaduni, mawazo, fikra n.k. Vyote hivyo havina mipaka ya kijiografia.

 1. MAMBO YA MSINGI KATIKA UTANDAWAZI

2.1       Utandawazi ni mfumo unaozipendelea nchi zilizoendelea. Na hali imekuwa hivyo tangu mahusiano na maingiliano ya kiuchumi kimataifa yaanze zaidi ya karne    tano zilizopita. Uhusiano kati ya nchi za Ulaya na Marekani na nchi za Dunia ya      Tatu umekuwa ni wa uporaji tu. Ukoloni ndio ulioimarisha mfumo huo wa uporaji     kwa kuamua makoloni yazalishe nini na kwa soko gani na kwa bei gani. Baada ya      uhuru, hali hiyo haikubadilika; mfumo wa uchumi ulibaki ule ule.

            2.2       Utandawazi ni mfumo ambao hatuna budi kuishi nao kwa:

(a)         Kutumia vizuri fursa unazotoa.

(b)         Kuyatumia hata mabaya yake kwa manufaa yetu.

Tunajifunza kuhusu utandawazi ili tutumie hata athari zake kwa manufaa yetu.

2.3       Nini kimeusukuma utandawazi

(i)                 Msukumo wa kibepari wa faida. Uchu wa mabepari wa kupata faida umesababisha mapinduzi makubwa katika uchumi. Soko la fedha na mitaji limekua na kujipenyeza kila mahali, na hasa katika nchi za Ulaya Mashariki, Asia na Marekani ya Kusini.

(ii)               Maendeleo katika sayansi na teknolojia ya:-

 1. a) Uzalishaji na huduma
 2. b) Habari na mawasiliano ambayo yamerahisisha sana biashara ya fedha, mitaji, bidhaa na huduma.

(iii)             Kuanguka kwa dola la Shirikisho la Kisovieti la Kisosholisti la Urusi (USSR) na washirika wake (nchi za Kijamaa za Ulaya Mashariki). Kitendo hicho kimeifanya dunia kuwa na itikadi moja, siasa ya demokrasia ya vyama vingi, mfumo mmoja wa uchumi (uchumi wa soko) na kuenea duniani kwa utamaduni wa Marekani na washirika wake. Nchi za Dunia ya Tatu na zilizokuwa za kikomunisti zipo katika hatua mbali mbali za utekelezaji wa marekebisho ya uchumi, ukiwemo ubinafsishaji wa mashirika ya umma.

(iv)              Matumizi ya nguvu za kisiasa katika kuendesha uchumi wa dunia. Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu (2000) inabaini: “….. Kutoweka kwa kambi ya Mashariki, kuenea kwa fikra, siasa na sera za uchumi za soko, na kuimarika kwa Kambi ya Magharibi, kumeleta mabadiliko makubwa katika diplomasia na mahusiano ya kimataifa. Nchi za kambi ya Magharibi hazina tena woga wala haya kuyaingilia madola mengine kwa kibali au, bila kibali cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Umoja ambao unatumiwa kama chombo cha sera za mambo ya nje ya mataifa makubwa.  Hata mabalozi wa nchi hizo katika nchi maskini wanaingilia mambo ya ndani ya nchi hizo kwa kisingizio cha kusimamia matumizi bora ya misaada yao. Kweli, Kujitawala ni kujitegemea” (Ibara ya 8).

Kuvamiwa na kukaliwa kwa Afghanistan na Iraq na majeshi ya Marekani         na washirika wake ni kiwango cha juu cha  ubeberu wa leo. Pia shughuli nyingi za kiuchumi husukumwa kisiasa ili kulinda na kuendeleza maslahi yao. Kuvunjika kwa mkutano wa Shirika la Biashara Duniani (World Trade Organization – WTO) kule Cancun mwezi Septemba 2003 kutokana na nchi matajiri kuendelea kung’ang’ ania kutoa ruzuku kwa wakulima wao huku nchi maskini zikikatazwa kufanya hivyo ni moja tu ya mifano ya matumizi ya hoja ya nguvu katika mahusiano ya kiuchumi, kwani, siasa ni uchumi.

 1. KWA NINI MANUFAA YA UTANDAWAZI KWETU NI MADOGO

3.1       Uhodhi wa nchi za magharibi wa mambo muhimu ya utandawazi.

Nchi za magharibi zinahodhi mambo yote muhimu ya utandawazi: teknolojia ya         uzalishaji, huduma, habari na mawasiliano; biashara; vyombo vya fedha; masoko  ya fedha na mitaji; n.k. Nchi hizo huelekeza raslimali kule ambako kunaleta faida  kubwa. Hakuna biashara ya kijamaa.

3.2       Uwezo wetu mdogo wa kumeneji (Kudhibiti) mabadiliko

Utandawazi ni mchakato wa mabadiliko katika nyanja zote za mfumo wa maisha  ya jamii. Menejimenti ya mchakato huo inahitaji ujuzi wa mfumo wenyewe; kuchanganua masuala yenye maslahi kwa nchi/taifa; dhamira ya kisiasa ya kuyakabili mabadiliko; na uzalendo.

Sisi tunakabiliana na utandawazi katika mazingira ya uchumi tegemezi,uliyonyuma na wa ukoloni mamboleo (Programu ya Chama cha Mapinduzi, 1987          – 2002).

Kutetereka kwa msingi wa uchumi wetu na kukithiri kwa umaskini ni sababu           kubwa ya kushindwa kwetu kuzitumia fursa zinazoletwa na utandawazi. Kanuni  ya Siasa Uchumi inasema kwamba  kama msingi wa uchumi ukitetereka, mahusiano yote ya kisiasa na kijamii (vikolombwezo) yanayumba: siasa, sera, utamaduni, ulinzi/usalama, sheria, mahakama, utawala bora, n.k. Mara nyingi sana, kwa kukosa ufahamu wa chimbuko la matatizo yetu tumekuwa tukitupiana lawama zisizo na msingi wowote, na hasa viongozi wa vyama vya upinzani. Viongozi wa vyama vya upinzani wamekuwa wakitoa ahadi rahisi za kilaghai kana kwamba wana dawa ya kutibu umaskini. Wanaifanya jamii  iamini  kuwa jukumu la kuleta maendeleo ni la serikali na Chama Tawala,  jambo  ambalo siyo kweli kabisa. Hakuna mtu anayeweza kuondoa umaskini wa  mwenzake. Anaweza kusaidia tu.

Baadhi ya mambo ambayo yamesababishwa na kuyumba kwa msingi wa uchumi    wetu na athari za utandawazi ni: (i) Kuongezeka kwa watu wasio na kazi; (ii) Kukua kwa sekta isiyo rasmi (wazalishaji na wafanyabiashara wadogo wadogo, machinga, mama/baba lishe, n.k.); (iii) Kuongezeka kwa uhalifu (na hasa ujambazi wa kutumia silaha, mauaji, biashara ya madawa ya kulevya, ubakaji, kutupa watoto wachanga, ukahaba, utapeli), (iv) ulimbukeni na kukosa uzalendo ambako kunasababisha fedha na mali nyingi za nchi kuporwa na wafanyabiashara  na wazalishaji wa nje, n.k. Wafanyabiashara wanaoagiza bidhaa kutoka nje na  kuigeuza nchi yetu dampo la bidhaa hafifu kutoka nje wakati bidhaa zetu zinakosa soko ni limbukeni wasio na uzalendo.  Au watumishi wa umma   wanaotia saini mikataba inayotukandamiza kwa sababu tu ya kupewa rushwa ni limbukeni – hawana uzalendo.  (v) Kuibuka kwa vyama vya siasa vya kitapeli na asasi zisizo za kiserikali.  Vyama vya siasa na asasi nyingi zisizo za kiserikali (NGOs) viliibuka ili kuikabili hali ngumu ya maisha iliyosababishwa na kuyumba         kwa uchumi.  Vilianzishwa ili kuganga njaa ndiyo maana hadi leo hakuna     dalili kama kweli vina lengo la kujenga demokrasia.

 1. CHAMA CHA MAPINDUZI NA SERIKALI ZAKE WAFANYE NINI ILI           KUNUFAIKA NA MFUMO WA UTANDAWAZI.

 

Kama tulivyoeleza hapo juu, hatuna budi kuzitumia fursa na changamoto zote             kwa manufaa yetu.  Azma hiyo inaweza kutekelezwa kwa kutumia sera, sheria, kanuni na taratibu.

 

            Njia kuu za Chama Tawala za uongozi ni kama ilivyo katika Mwongozo wa     TANU (1971):           

 

(a)               Kutoa lengo; yaani kuandaa sera.

(b)               Kuwaandaa watekelezaji wa sera hizo; ambao ni serikali na vyombo vyake; asasi zisizo za kiserikali; vyama na asasi za kijamii; na wananchi, wakulima, wafanyakazi, wafanyabiashara, wanaume, wanawake na watoto.

(c)               Kusimamia utekelezaji wa sera zake (ufuatiliaji, uhimizaji, masahihisho, n.k.)

(d)               Kupima (kutathmini) matokeo ya utekelezaji wa sera kwa lengo la kubaini mapungufu na kufanya marekebisho ya kisera.

Majukumu hayo ya Chama Tawala bado yana umuhimu leo kama ilivyo           kuwa mwaka 1971. Hii ndiyo tafsiri ya Chama Kutawala/Kuongoza.

 

Zaidi ya majukumu hayo ya kisera, Chama Tawala pia kina nafasi kubwa ya kuendesha elimu ya umma  (advocacy) kuhusu masuala nyeti kama vita dhidi ya UKIMWI, unyanyasaji wa kijinsia, mmomonyoko wa           maadili katika jamii, ajira ya watoto, n.k.  Kwa hiyo basi, kuhusu utandawazi, Chama cha Mapinduzi kinaweza kuongoza Serikali zake             kupitia sera na jamii kupitia elimu ya umma (advocacy).

 

4.1       Sera kama njia ya Chama ya Uongozi.

Vyama vya TANU, ASP na CCM vimejijengea sifa kubwa sana ya kuwa na sera  safi katika nyanja zote za maisha ya jamii na Taifa.  Hatuna sababu ya kuziorodhesha hapa.  Na Serikali za CCM zimeandaa sera mbalimbali za utekelezaji wa Mwelekeo wa CCM katika miaka ya 1990 na 2000 – 2010 na Ilani za CCM za Chaguzi Kuu za mwaka 1995 na 2000.  Hivi sasa serikali inakamilisha Sera ya Taifa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.  Tume ya Dunia Kuhusu Athari za Kijamii za Utandawazi imebaini kwamba nchi za Dunia ya Tatu (Maskini) zimeathirika sana katika maeneo yafuatayo:

 

(a)               Mfumo wa dunia wa uzalishaji ambao umezifanya ziendelee kuzalisha na kuuza nje bidhaa ghafi ambazo bei zake huendelea kushuka katika soko la dunia.

(b)               Utegemezi wa bidhaa za viwanda na teknolojia ya kisasa katika uzalishaji na huduma.

(c)               Ongezeko kubwa la idadi ya watu wasio na kazi, na hasa vijana.  Katika Tanzania tumefikia hali kwamba vijana wanaomaliza elimu ya juu hawana uhakika wa ajira.  Kitengo cha Kuondoa Umaskini na Ajira katika Idara ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi na Ustawi wa Jamii kinakadiria kuwa vijana milioni 188, wengi wao kutoka nchi zinazoendelea wanaishi bila kufanya kazi, au kufanya kazi za kipato kidogo (Kaale, katika Majira Jumapili, Julai 11, 2004; Tume ya Utandawazi, uk.40).

(d)               Kuwafanyisha kazi watoto wa chini ya miaka 15, hivyo kuwakosesha elimu na kuwaingiza katika mzunguko usio na mwisho wa umaskini na dhiki.

(e)               Athari katika utamaduni wetu.  Ingawaje Tanzania ina Sera ya Taifa ya Utamaduni, athari za utandawazi katika jamii, na hasa kuiga tamaduni za Magharibi, ni za kutisha.  Vyombo vya upashanaji habari na mawasiliano (redio, magazeti, hasa ya udaku, TV, intaneti, n.k.) vimekuwa mbadala wa wazazi na watu wengine wazima katika jamii katika malezi ya watoto.  Uhuru wa kutoa maoni umegeuka kuwa huria (anarchy) katika kutafuta habari na kutoa maoni na hasa kuiga tamaduni za kigeni.

 

Kwa kiwango kikubwa, yafuatayo ama yameletwa au kuchochewa na utandawazi:

 

 • mmomonyoko wa maadili katika jamii (kutoweka kwa adabu na heshima miongoni mwa watoto, vijana na baadhi ya watu wazima);
 • tamaa ya utajiri wa haraka haraka ambayo imeondoa uaminifu/juhudi katika kazi na kuleta uhalifu wa kutumia silaha, utapeli, uingizaji wa bidhaa hafifu nchini;
 • nyanja ya starehe na burudani imetawaliwa na matendo yanayoibua hisia za ngono na kuchochea ufuska hivyo kuyafanya mapambano dhidi ya UKIMWI kuwa kama mchezo wa kuigiza. Hata baadhi ya matangazo yenye lengo la kudhibiti maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU) yanachochea ngono kinyume na matarajio.
 • Kuibuka kwa vyama vya siasa na asasi zisizo za kiserikali ambavyo huchochea vurugu na uvunjifu wa sheria na mshikamano wa kitaifa.

 

4.2       Maeneo muhimu kisera.

Kuhusu utandawazi, maeneo muhimu kisera ni kama ifuatavyo:

 

(i)         Uhusiano wa kimataifa.

Kama ilivyoelezwa, utandawazi ni mahusiano na mwingiliano wa kimataifa.  Sera ya sasa ya Taifa ya Uhusiano wa Kimataifa inakidhi mahitaji yote muhimu ambayo yanajenga mazingira mazuri kwa Tanzania kunufaika na utandawazi.  Sera hiyo inasisitiza umuhimu wa ujirani    mwema; kukuza ushirikiano wa kieneo (k.m. Jumuiya ya Afrika             Mashariki); kikanda (k.m. Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC); na ushirikiano baina ya nchi za kusini (South – South           cooperation).

 

Aidha, sera inazitaka ofisi zetu za ubalozi kuwa watangazaji wa utajiri wa kiraslimali wa nchi yetu ili kuwavutia wawekezaji, na watalii na kutafuta masoko kwa bidhaa zetu.   Uhusiano wa kimataifa ulenge masoko na vyanzo vya teknolojia ya kisasa.

 

(ii)        Uchumi na Maendeleo.

(a)       Ubinafsishaji

Jukumu katika eneo hili ni kuhakikisha kwamba Taifa linanufaika       na manufaa hayo yanawafikia walio wengi.

(b)       Kupambana na ukosefu wa ajira

Serikali zina mipango na programu madhubuti za kuondoa umaskini.  Jitihada hizo hazina budi kupongezwa.

Hata hivyo, suala la ukosefu wa ajira halinabudi kuundiwa mkakati maalumu hasa kutokana na uhusiano wake na amani na usalama wa Taifa.  Mambo ya kisera:

 

 • Kuainisha ajira katika mazingira ya Tanzania. Ajira kuu ya Watanzania ni kilimo, siyo viwanda. “Siasa ni Kilimo” (TANU, 1972).

 

 • Kuwahamasisha wanaojiajiri (kwa kuwapunguzia kodi, mikopo yenye riba nafuu).
 • Kuwashirikisha vijana wenyewe kutaka kubuni na kupanga mikakati ya ajira.

 

Kaale (kama hapo juu) anamnukuu Katibu wa Mtandao wa Umoja wa Mataifa wa Ajira kwa Vijana (Youth Employment Network – YEN), Bw. Steve Miller akisema:

 

“Kwa mujibu wa makubaliano ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kila nchi itaunda mtandao wa ajira kwa             vijana utakaojumuisha Taasisi za Serikali, Mashirika ya             Kimataifa, Taasisi za Elimu, vikundi vya vijana, wasomi,          sekta isiyorasmi, taasisi za fedha, asasi zisizo za kiserikali,      vyombo vya habari na wadau wengine wakereketwa wa    maendeleo ya vijana.”

 

Tanzania imekwishaunda Mtandao wa Taifa wa Ajira kwa Vijana.  Lakini, ili vijana washiriki katika mtandao huo, wanahitaji hali ya utulivu wa kisiasa na kuamini kwamba suala hilo halina mfungamano na itikadi za kisiasa.

 

Mchakato wa kupambana na tatizo la ajira hauna  budi kwenda sambamba na mapambano dhidi ya ajira ya watoto.

 • Kuheshimu haki za wafanyakazi

Tangu enzi za kupigania uhuru, vyama vya TANU, ASP na         sasa CCM vilikuwa na mfungamano mkubwa na             wafanyakazi kupitia vyama vyao.

 

Ingawaje utandawazi unarembwa na lugha ya mapinduzi ya demokrasia, utawala bora, utawala wa sheria, haki za binadamu, na kadhalika, katika hali halisi ni mfumo wa kibabe na dhuluma.  Baadhi ya waajiri huwapiga marufuku wafanyakazi wao kujiunga na vyama vya wafanyakazi.

 

(c)        Uzalishaji na Utoaji Huduma

Mwelekeo wa sera za CCM katika Miaka ya 2000 hadi 2010           umetamka kwamba Modenaizesheni ndiyo mkakati wa ujenzi wa            msingi wa uchumi wa kisasa wa taifa linalojitegemea (Ibara ya             20). Mkakati huo pia utaongoza maendeleo katika miundombinu ya kiuchumi na kijamii.

 

Katika suala la uzalishaji wa bidhaa za kuuza nje (hata ndani), mambo ya kuzingatiwa ni:

 • kuuza bidhaa zilizosindikwa badala ya bidhaa ghafi.
 • Aina za mazao. Kuzalisha kwa wingi mazao yenye bei kubwa kwenye soko.
 • Ubora wa mazao. Ushindani mkubwa katika soko la dunia unahusu ubora wa bidhaa.
 • Kuangalia mwenendo wa bei katika soko la dunia. Haileti faida kuzalisha mazao ambayo yana bei ndogo.
 • Utafutaji wa masoko mapya na kuwa na mikataba ya ununuzi na uuzaji.

(d)       Katika miaka ya 1970 na 1980, Tanzania ilikuwa na sera ya maendeleo ya viwanda.  Viwanda vinavyozalisha bidhaa muhimu kama chuma, kemikali, ngozi, karatasi, viatu na hata nguo vingi vimefungwa.  Ingawaje kwa hivi sasa kilimo ndiyo sekta kiongozi, viwanda ndivyo vitakuwa mhimili wa uchumi wetu. Kilimo cha kisasa kinategemea sana mazao ya viwandani.   Kukuza  viwanda vya msingi vya kuzalisha mashine na vifaa kunahitaji chuma.  Chuma Cha Mapinduzi hakina budi kuwa na sera kuhusu uchumbaji wa makaa ya mawe na chuma.

 

(e)       Masuala mengine ya kiuchumi

 • Uchimbaji wa madini;
 • Utalii;
 • Uvuvi na biashara ya nje ya samaki;

 

Vyote hivyo vilenge kulinufaisha Taifa na siyo kuwatajirisha wawekezaji tu.

 

(f)        Huduma za Jamii

Katika huduma za jamii, Mwelekeo wa sera za CCM katika Miaka ya 2000 hadi 2010 unaweka mkazo mkubwa katika maendeleo ya Elimu, na hasa sayansi na teknolojia (ufundi).  Mkazo uwe katika utafiti ambao utaongeza ufanisi na tija katika nyanja zote za uzalishaji na utoaji huduma.  Mapinduzi katika elimu, na hasa sayansi na teknolojia yametiliwa mkazo sana na Tume ya Utandawazi.

 

Hivi sasa, utafiti katika vyuo vikuu hufadhiliwa na wahisani.  Wahisani hao huchagua hata aina ya utafiti na wapi ufanyike.  Lazima tujikwamue kutokana na utegemezi wa aina hii unaozaa wataalamu tegemezi hata katika kufikiri.

 

(g)       Utawala  bora

Utawala bora unaojali haki za binadamu na kwamba kila raia ni sawa mbele ya sheria, unaoheshimu uhuru wa mahakama na unaopambana na maovu kama rushwa, unaelezwa kuwa msingi wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.  Kwamba, bila utawala bora, hakuna maendeleo.

 

Hakuna ubishi kwamba serikali ya Tanzania inazingatia misingi yote ya utawala bora.  Rais mwenyewe ni Waziri wa Utawala Bora akisaidiwa na Waziri wa Nchi.  Pia, serikali inaandaa sera ya haki za binadamu.

 

4.3       Utandawazi na kupungua kwa madaraka na mamlaka ya serikali.

 

Taarifa ya Tume ya Dunia kuhusu Athari za kijamii za Utandawazi imebaini kwamba mageuzi ya kiuchumi na kisiasa ndani ya utandawazi yamepunguza sana mamlaka na madaraka ya serikali katika nchi zinazoendelea ambayo ni muhimu sana katika kuunda na kusimamia utekelezaji wa sera.  Mamlaka na madaraka ya serikali yamepunguzwa na:

 • “kujitoa” kwa serikali katika kuendesha uchumi.
 • Makelele ya vyama vya upinzani ambavyo havina sera lakini vina uchu wa kutawala.
 • Asasi zisizo za kiserikali ambazo zinajipa sauti ya kisiasa kwa ruzuku kutoka nje. Hakuna aliyepima mchango wa asasi hizo katika maendeleo ya jamii hasa ikilinganishwa na fedha wanazopewa na wahisani, pengine kwa shabaha za kisiasa.
 • Kampeni za wanasiasa na asasi mbalimbali zisizo za kiserikali hasa kuhusu haki za binadamu, utawala wa sheria ambazo zimepandisha kiwango cha utambuzi wa jamii (social consciousness) baina ya wananchi wengi; hali inayochochea maasi dhidi ya sheria, kanuni na taratibu. Kwa mfano, vyama vya siasa kudai mabadiliko ya Katiba (kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi) kwa njia ya maandamano ambayo ni mamlaka na madaraka ya Bunge. Serikali hazina budi kulinda haki zake za utawala wa nchi.  Wanaotaka kutawala wasubiri wapewe ridhaa na wananchi.  Serikali ina kazi moja tu:  kutekeleza sera na Ilani ya CCM.

 

4.4       Chama na Usimamizi, ufuatiliaji wa utekelezaji wa sera zake.

 

Ingawaje mara nyingi kuna pengo kati ya sera na utekelezaji wake, vyama vyetu         havina sifa nzuri sana katika suala la usimamizi na ufuatiliaji wa utekelezaji wa sera.  Hali ilikuwa hivyo wakati wa mfumo wa chama kimoja. Ingawaje vyama vya TANU, ASP na CCM vilisimamia utekelezaji wa sera  zake moja kwa moja, bado mapungufu yalikuwa mengi.  Sera zilibadilishwa hata             bila kufanyiwa tathmini ili kubaini mafanikio na matatizo.

 

Baada ya kuingia katika mfumo wa vyama vingi, sasa usimamizi hufanywa na         vyombo vya uwakilishi ambavyo hata wakati wa mfumo wa chama kimoja  vilifanya kazi hizo hizo.  Vyombo hivyo ni Bunge, mabaraza ya maendeleo ya kata, halmashauri za wilaya, miji, manispaa na jiji.

 

Kwa maoni yetu, Chama Tawala hakiwezi kubaki na jukumu la kuunda sera na kuviachia vyombo vingine kazi za maandalizi ya umma, usimamizi na tathmini. Wakati wa utekelezaji wa Siasa ni Kilimo (TANU, 1972), uhamasishaji ulioongozwa na kusimamiwa na Chama  uliongeza uwingi na ubora wa mazao ya chakula na biashara.  Serikali na vyombo vya uwakilishi haviwezi kuwa mbadala wa Chama Tawala katika maandalizi ya umma, usimamizi na tathmini  ya utekelezaji.  Wala chama hakiwezi kuwa karibu na wanachama na wananchi  isipokuwa kupitia kazi za kisiasa za maendeleo, ustawi wa jamii, ulinzi na usalama.  Chama cha Mapinduzi kisipofanya hayo, vyama vya upinzani vitaziba pengo.  Wapinzani wanatoa madai ya kipuuzi kwamba viongozi wa CCM (wakiwemo wabunge) hawajafanya kitu kwa sababu viongozi wa CCM hawasemi  Chama na Serikali zake wamefanya nini.

 

5                    MAMBO MENGINE MUHIMU KATIKA UTANDAWAZI.

 

5.1       Uwezo wa majadiliano (negotiation)

Kunufaika na mikataba ya kimataifa kunategemea sana uwezo wetu wa majadiliano (negotiation). Majadiliano hayo yanahitaji ufahamu wa masuala husika na msimamo wa kizalendo (kuweka mbele maslahi ya Taifa kabla ya binafsi).  Hatuna budi kujidhatiti katika hilo.

 

 

 

 

5.2       CCM kutumia teknohama

Mtandao wa uongozi wa Chama cha Mapinduzi unaoanzia ngazi ya shina hadi         Taifa ungenufaika sana kama ungeunganishwa na mtandao wa mawasiliano wa kompyuta.  Tunafahamu kwamba Makao Makuu ya CCM yameunganishwa  kwenye intaneti na yana tovuti yake. Jitihada ifanyike ili mikoa na wilaya kwa        kuanzia iunganishwe kwenye matandao wa kompyuta ili kurahisisha mawasiliano        ndani ya chama.

 

 1. HITIMISHO

Ingawaje ni kweli kwamba utandawazi wakati wote umezipendelea nchi zilizoendelea ambazo zinahodhi sayansi na teknolojia, bado kuna nafasi kwa nchi  zinazoendelea kunufaika na mfumo huo.  Chama cha Mapinduzi kina uwezo wa kuongoza mchakato wa kuifanya Tanzania kunufaika na mfumo wa utandawazi.  Akizungumza kwenye mkutano wa kwanza wa Umoja wa Afrika, Durban, 9 Julai, 2002, Rais Benjamin Mkapa, Mwenyekiti Mwenza wa Tume ya Dunia            kuhusu Athari za Kijamii za Utandawazi, alimnukuu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye alitoa maneno yafuatayo ya Kizanaki wakati wa uzinduzi wa   Tume ya Kusini tarehe 20 Oktoba, 1987:

 

‘Wakasusu, nihe wagya?

Nagya kwita Wanzugu.

Oragya kutura?

Ndagya Kusaya-sayamu, Ndinukira!

 

Maana yake:

 

‘Sungura, unakwenda wapi?

Nakwenda kumwua tembo.

Utaweza?

Ah, nitajaribu na nitajaribu tena.

 

Rais Mkapa alisisitiza kwamba Nchi za Kusini zisikate tamaa. Tunasisitiza,

 

tusikate tamaa.

REJEA.

 1. Semboja, J., Mwapachu, J. and Jansen, E. (2002), Local Perspectives on Globalisation:The African Case, Dar es Salaam:  Mkuki na Nyota Publishers.

 

 1. Mkapa, B.W. “Statement at the Launching of the National Dialogue on the SocialDimension of Globalisation,” Golden Tulip Hotel, 19 August, 2002.

 

 1. URT (2002), President Benjamin William Mkapa Speaks on the Social Dimension of Globalisation, Dar es Salaam:  Government Printer.

 

 1. Kent, Bruce (1991), Bulding the Global Village, Glosgow:Harper Collins.

 

 1. Rosenan, James, N. “Globalization and Governance:Bleak Prospects for                  Sustainability,” In: International Politics and Society, Vol.3, 2003.

 

 1. Shao, Ibrahim, F. (2003), “Utandawazi na Nchi Maskini,”Makala iliyotolewa kwenye Semina ya Wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Zanzibar  14/1/2003.

 

 1. Kapinga, D.S. (2003), Globalisation: Its Evolution and Changed Perspectives, Processed, DSI, SUA.

 

 1. World Commission on the Social Dimension of Globalisation (2004),A FAIR            GLOBALISATION:  CREATING OPPORTUNITIES FOR ALL, Geneva: ILO.