Tumeachanamapuri

JEE, TUMEACHANA NA SIASA YA UJAMAA NA KUJITEGEMEA? LA HASHA

 

[Na Omar R. Mapuri]

 

UTANGULIZI:

 

Tokea mwanzoni mwa miaka ya tisini, Tanzania imo katika mageuzi makubwa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ambayo yanakwenda sambamba.  Mageuzi ya kisiasa yametuingiza katika mfumo wa vyama vingi vya siasa baada ya zaidi ya miaka 40 ya mfumo wa chama kimoja.  Mageuzi ya kiuchumi yametutoa katika uchumi hodhi uliokuwa ukimilikiwa na dola na kutuingiza katika mfumo wa uchumi wa soko unaotoa nafasi ya ushiriki wa sekta ya  binafsi.  Mageuzi ya kijamii ni pamoja na kupanuka kwa uhuru wa vyombo vya habari pamoja na mambo mengine mengi ambayo aghlabu ni matokeo ya mageuzi ya kiuchumi na kisiasa.

 

Kama ilivyo kawaida ya mageuzi, mageuzi haya makubwa na mengi yanayokwenda sambamba yamewafadhaisha na hata kuwababaisha wananchi wengi wakiwemo wana CCM.  Ilivyokuwa mageuzi hayo yameletwa, yanaendeshwa  na kusimamiwa na CCM, wapo wana CCM wanaojiuliza kama CCM imeachana na sera zake za msingi, hasa Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea na dira ya utekelezaji wake ambayo ni Azimio la Arusha.  Wapo pia wanachama wa CCM wachache, wakiwemo hata viongozi, ambao hawajiulizi tena, bali wanaamini hasa kwamba CCM imekwishaachana na sera zake.  Katika nyakati fulani wapo hata viongozi wa CCM waliosikika wakitoa kauli kama vile:  “tulipokuwa tukijenga ujamaa ….” au “enzi zile za Azimio la Arusha ….” kama vile ujenzi wa ujamaa haupo tena au enzi za Azimio la Arusha zimekwisha.  Yupo hata kiongozi mkubwa wa CCM aliyewahi kutamka mwanzoni mwa vuguvugu la mageuzi kwamba eti CCM haina dira. Aidha, wapo wasomi wanaojaribu kuonyesha kwamba CCM imeachana  na ujamaa na kwamba sasa inaendesha sera wanazoziita za kiliberali.  Zaidi ya yote, vipo hata vyama vya upinzani vilivyodiriki kujinasibu kwamba eti vyenyewe ndivyo sasa vyenye sera za ujamaa  eti kuziba pengo lililoachwa na CCM iliyoutelekeza ujamaa.

 

Katika makala haya tutajaribu kusahihisha dhana hizo ambazo tunaamini kwa kiasi kikubwa ni matokeo tu ya ubabaikaji uliosababishwa na mageuzi. Tutajitahidi kuonyesha kwamba CCM haijaachana na siasa yake ya Ujamaa na Kujitegemea, bali ambacho kimekuwa kikibadilika kulingana na wakati na mazingira, ni mikakati tu ya kufikia lengo hilo kuu la muda mrefu.

 

UCHANGANUZI WA MANENO ”FALSAFA”, “IMANI”, “SIASA”, “SERA”, “ILANI” n.k.

 

Kabla ya kuitazama kwa undani siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, inafaa kwanza kuchanganua maneno ya “falsafa”, “imani”, “siasa”, “itikadi”, “sera”, “maamuzi” na “ilani” ambayo yanatumika sana katika kuielezea dhana nzima ya ujamaa na kujitegemea katika mikutadha mbali mbali.

 

Falsafa:

 

Falsafa inayosarifu dhana na nadharia za Chama Cha Mapinduzi, na nchi nzima kwa jumla ni usawa wa binadamu na mtu kuthaminiwa kwa utu wake.  Falsafa hii inabeba dhana za uhuru, demokrasia, haki, udugu na amani.  Falsafa hii inaashiriwa katika Ahadi ya Kwanza ya Mwanachama wa CCM isemayo: “Binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja”.  Falsafa hii ndiyo pia iliyoweka misingi ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Zanzibar.  Katika Utangulizi wa Katiba zote mbili unapata maneno yafuatayo: “… tumeamua rasmi na kwa dhati kujenga katika nchi yetu jamii inayozingatia misingi ya uhuru, haki, udugu na amani.”  Pia Katiba hizo zinaendelea: “…. Misingi hiyo yaweza tu kutekelezwa katika jamii yenye demokrasia …”  Ibara ya 12 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haikuvunga vunga maneno katika kuibainisha falsafa hii ya msingi.  Ibara hiyo inasomeka kama ifuatavyo:-

 

 

 

 

“12. – (1)   Binadamu wote huzaliwa huru, na wote ni sawa.

(2) Kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake.

 

Ibara ya 11 ya Katiba ya Zanzibar ina maneno hayo hayo.

 

Inathibitika kwa hivyo kwamba falsafa hii si ya CCM peke yake, bali ni ya nchi nzima.  Hatujapata kusikia chama hata kimoja cha siasa kinachoipinga falsafa hii.

 

Imani/Siasa/Itikadi:

 

Ni imani ya CCM kwamba ujamaa na kujitegemea ndiyo njia pekee ya kujenga nchi ya watu walio sawa, huru na wanaoheshimiana.  Kwa hivyo, hiyo ndiyo siasa  au itikadi ya msingi ya CCM.  Ibara ya 4 ya Katiba ya CCM inaweka bayana imani ya CCM kama ifuatavyo:-

 

 1. CCM kinaamini kwamba:

 

(1)    Binadamu wote ni sawa

(2)    Kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake.

(3)    Ujamaa na kujitegemea ndiyo njia pekee ya kujenga jamii ya watu walio sawa na huru

 

Kwa upande wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sehemu ya Utangulizi imeelezea madhumuni ya kutungwa kwa Katiba hiyo kuwa ni kujenga jamii yenye demokrasia na pia kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Tanzania inaongozwa na Serikali yenye kufuata misingi ya demokrasia na ujamaa.  Maneno kama hayo yamerejewa pia katika Katiba ya Zanzibar.

 

Ibara ya 3(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaitangaza rasmi Tanzania kuwa ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamaa, yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa. Ibara ya 8(1) ya Katiba ya Zanzibar nayo imeitangaza hivyo hivyo Zanzibar isipokuwa tu imetumia maneno “haki za kijamii” badala ya neno “ujamaa”.  Hata hivyo madhumuni ni yale yale.

 

 

 

Tukizilinganisha Katiba za nchi na ile ya CCM katika muktadha wa siasa ya ujamaa na kujitegemea, inadhihirika kwamba neno “kujitegemea” halikutumika katika Katiba za nchi.  Tafsiri yetu ya tofauti hiyo ni kwamba katika siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, ncha ya ujamaa ni ya nchi nzima lakini ncha ya kujitegemea inatoa fursa kwa vyama vya siasa kutofautiana kwa sera.  Ingawa kuna vyama vya upinzani ambavyo husikika vikitaka kipengele cha Ujamaa kiondoshwe katika Katiba ya nchi, lakini ukizitazama kwa undani sera za vyama hivyo, utagundua kwamba zimejengwa juu ya msingi huo huo wa ujamaa.  Na vipo vyama ambavyo hujinasibu kwa wananchi kwamba eti ndivyo vyenye uwezo mkubwa  zaidi wa kuzitekeleza sera za CCM kuliko CCM yenyewe.  Vyama kama hivyo vinakiri usahihi wa siasa ya Ujamaa lakini vinadai kuwa eti CCM haina uwezo wa kuitekeleza.  Lakini zaidi ya yote, hatujapata kusikia chama cho chote cha siasa nchini Tanzania kinachojitambulisha na ubepari.

 

Sera na Dira:

 

Baada ya kubainisha siasa yake ya Ujamaa na Kujitegemea iliyojengwa juu ya msingi wa  falsafa ya usawa wa binadamu na mtu kuthaminiwa  kwa utu wake, TANU mnamo mwaka wa 1967 ilipitisha Azimio la Arusha lililoandaa mazingira  na kuweka dira ya utekelezaji wa siasa hiyo.  Sera ni  mkakati wa utekelezaji wa siasa kwa kipindi fulani kulingana na uchambuzi wa dira uliofanywa kwa ajili ya kipindi hicho.  Sera huweza kubadilika kulingana na mahitaji ya wakati.  Kwa hivyo, wakati siasa ya Ujamaa na Kujitegemea ni ya kudumu na Azimio la Arusha  kama dira yake ya utekelezaji nalo ni la kudumu kwa kiasi fulani, sera na mikakati ya utekelezaji huweza kubadilika kila baada ya muda, kulingana na mabadiliko ya mahitaji ya wakati.   Na kweli uzoefu katika TANU na ASP na baadaye CCM unaonyesha kwamba baada ya kila kipindi cha wastani wa miaka 10, Chama kimekuwa kikitathmini utekelezaji wa siasa ya Chama na kuzitazama upya sera zake za msingi kwa lengo la kuzifanya zikidhi mahitaji ya wakati.  Baada ya kufanya mapitio hayo Chama huja ama na mwongozo unaojikita katika ufafanuzi na kuyawekea mkazo maeneo fulani au huja na sera mpya kabisa,  lakini lengo kuu likiwa ni lile lile la kutekeleza siasa ya Ujamaa na Kujitegemea kwa kuzingatia misingi ya Azimio la Arusha.  Ndiyo maana katika kipindi cha toka 1971 hadi sasa, CCM imetoa nyaraka nne zifuatazo za kisera za msingi:-

 

(1)            Mwongozo wa TANU wa 1971 ambao ulijenga hamasa ya utekelezaji wa Azimio la Arusha.

 

(2)              Mwongozo wa  CCM wa 1981 ambao ulijielekeza katika kukabiliana na mmong’onyoko wa maadili uliokuwa unasababishwa na hali ngumu ya uchumi iliyochangiwa na vita vya nduli Idi Amin.

 

(3)            Mwelekeo wa Sera za CCM katika Miaka ya Tisini
uliozingatia haja ya kujihami na taathira za upepo wa mageuzi makubwa ya kiuchumi na kisiasa uliokuwa ukivuma Duniani na kuziangusha dola kubwa za kijamaa za Ulaya ya Mashariki likiwemo la Urusi yenyewe ya Kisovieti.

 

(4)            Mwelekeo wa Sera za CCM katika Miaka ya 2000-2010 unaozingatia zaidi suala la matumizi ya teknolojia (modenaizesheni) katika ujenzi wa uchumi wa kisasa.

 

Kwa jumla, chimbuko la sera zote za CCM ni Azimio la Arusha na zinapoandaliwa, yanazingatiwa pia malengo na madhumuni ya CCM yaliyobainishwa katika ibara ya 5 ya Katiba ya CCM.  Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere katika “Kujitawala ni Kujitegemea” aliyaelezea ifuatavyo mahusiano baina ya Azimio la Arusha na Sera za Chama:-

 

Azimio la Arusha ndilo linaloeleza itikadi ya chama chetu.  Ndiyo kauli kuu ya lengo letu na misingi yetu; ndilo msingi wa maamuzi yote ya sera za Chama na Serikali.

 

Aidha Mwalimu alitambua haja ya kupitia upya sera kila mara na kurekebisha Azimio.  Alisema tena katika “Kujitawala ni Kujitegemea:-

Kila miaka inavyopita, kauli yo yote muhimu kupitiwa mara kwa mara kuona kama misingi yake bado inahitajiwa katika mazingira mapya …  Hata mimi nakubali kwamba (Azimio la Arusha) linahitaji marekebisho.

 

Maneno hayo yanatosha kuwasuta wale wanaodai kwamba eti Mwalimu hakutaka mabadiliko ya Azimio na Sera.

 

Maamuzi:

 

 Ndani ya utekelezaji wa sera ya msingi, Chama huweza kupitisha maamuzi yenye lengo la kutoa msukumo wa utekelezaji wa jambo fulani mahsusi au kukabili tatizo fulani la utekelezaji.  Ni kwa msingi huo ndio TANU na baadaye CCM ilipitisha maamuzi mengi yakiwemo yafuatayo:-

 

(1)            Siasa ni kilimo (Azimio la Iringa) (1972) kwa lengo la kutoa msukumo katika suala zima la kilimo.

 

(2)            Mpango wa Elimu kwa Wote (UPE) (Azimio la Musoma), (1974) uliotoa msukumo wa kuharakisha kufikisha elimu kwa wote ikiwa ni pamoja na suala la elimu ya watu wazima.

 

(3)            Mtu ni Afya (1976): Kutoa msukumo kwa sera ya kinga kuliko tiba.

 

(4)            Mpango wa Kujihami Kiuchumi (1980/81) ili kukabiliana na hali ngumu ya uchumi wa nchi.

 

(5)            Maamuzi ya Zanzibar (1991) ambayo yaliwaondolea wanachama wa kawaida wa CCM masharti ya uongozi yaliyoainishwa katika Azimio la Arusha.  Maamuzi hayo yalikuwa na lengo la kuwawezesha wanachama wa CCM kushiriki katika harakati za kiuchumi katika mazingira mapya yaliyokuwa yanaingia ya uchumi wa soko.  Masharti ya uongozi yalibaki kwa viongozi tu kama ilivyokuwa imekusudiwa katika Azimio la Arusha.

 

Ilani:

 

Kama ilivyokwishabainishwa, sera za msingi huchukua upeo wa muda mrefu kidogo, na kwa uzoefu wa CCM, ni kama miaka 10 hivi.  Ndani ya kipindi hicho, Chama huchambua sera na kujipangia malengo ya utekelezaji kwa vipindi vifupi vifupi, aghlabu vya miaka mitano mitano.  Hapo ndipo tunapopata ilani za uchaguzi ambazo huwasilishwa kwa wananchi kwa ajili ya kuombea kura katika chaguzi za dola ambazo hufanywa kila baada ya miaka mitano.

 

Baada  ya uchanganuzi huo wa maneno “falsafa”, “siasa”, “itikadi” “sera”, “maamuzi” na “ilani”  kama yanavyotumika katika msamiati wa CCM, imedhihirika kwamba falsafa na siasa ni vitu vya kudumu, au ni malengo ya muda mrefu, lakini sera, maamuzi na ilani ni vitu vinavyobadilika kila baada ya muda.  Na hapa ndipo penye siri ya mafanikio ya CCM.  Ingawa CCM ni chama kikongwe, lakini kila baada ya muda hujirekebisha kwa mujibu wa mazingira ya wakati, lakini bila ya kupoteza lengo.  Kwa ufupi, CCM inafuata kanuni ya mwezi ambao katika mzunguko wake huanza na uchanga (ukiwa na umbo la hilali), ukafikia upevu (ukiwa na umbo la sahani) na kurejea tena uchanga ambapo unakuwa tunu tena.  Ni kutokana na kanuni hiyo ndiyo maana wananchi hawaichoki CCM pamoja na ukongwe wake, kwani wakati wote inawaletea matumaini mapya.

 

UJAMAA NA KUJITEGEMEA KAMA SIASA YA CHAMA:

 

Kama siasa ya Chama, Ujamaa na Kujitegemea ni lengo la kudumu.  Ni kwa msingi huo ndiyo tunasema kwamba Chama Cha Mapinduzi bado kabisa hakijaachana na siasa hiyo.  Katiba na sera za CCM zinabainisha  wazi wazi msimamo huo kama ilivyokwishaelezewa.  Baada ya kuuelewa msimamo huo, ni muhimu pia kuelewa tunapozungumzia Ujamaa na Kujitegemea tunakusudia nini.  Tutajaribu kwa kutumia lugha nyepesi kabisa, kutoa ufafanuzi huo katika sehemu hii ya makala haya.  Kama inavyojieleza yenyewe, siasa ya Ujamaa na Kujitegemea ina ncha mbili, yaani ya Ujamaa na ile ya Kujitegemea. Katika Azimio la Arusha, umefanywa uchanganuzi wa kina ambapo Sehemu ya Pili ya Azimio hilo inachambua Siasa ya Ujamaa na Sehemu ya Tatu inachambua Siasa ya Kujitegemea.  Kwa maneno mengine siasa yetu hii ni siasa mbili ndani ya moja.  Nasi kwa ufupi kabisa tutafanya uchanganuzi kama huo.

 

Siasa ya Ujamaa:

 

Siasa ya Ujamaa imechambuliwa na wanafalsafa wengi wakubwa waDunia hii wakiongozwa na Karl Marx na Vladmir Lenin.  Pia imechambuliwa kwa kina na Mwalimu Julius K. Nyerere kwa mazingira ya Tanzania katika vitabu vyake mbali mbali, ambapo majumuisho yake yaliwekwa katika Azimio la Arusha.  Sisi katika makala haya hatukusudii kurejea uchambuzi wa kifalsafa bali tu tunajaribu kumwelezea mwananchi wa kawaida maana pana na nyepesi inayokusudiwa katika Siasa ya Ujamaa.  Kwetu sisi Ujamaa maana yake ni kugawana utajiri wa nchi kwa usawa na kwa haki katika misingi ya kuheshimiana.  Jitihada zetu za kiutekelezaji katika kufikia lengo hilo kama zinavyoongozwa na Azimio la Arusha zimekuwa zikichukua sura za kusambaza huduma za jamii (elimu, afya, maji n.k.) kwa wote, kujenga misingi ya fursa sawa za kujiendeleza, kuondoa unyonyaji, kupiga vita kila aina ya ubaguzi na dharau, kuwatetea wanyonge na kuwasaidia kujikwamua na kadhalika.  Uamuzi wa kuanzisha vijiji vya ujamaa katika miaka ya sabini ulikuwa na lengo la kurahisisha utekelezaji wa juhudi hizi.  Pamoja na matatizo ya hapa na pale ya utekelezaji, tunaamini Watanzania walio wengi hasa wanyonge, bado wanapenda kufikiwa kwa malengo hayo.  Ndiyo maana tunasema Siasa ya Ujamaa ni ya kudumu.

 

Kugawana au kusambaza kwa wote utajiri wa nchi (si kwa kugawana fedha bali kwa kuhakikisha upatikanaji wa huduma za kijamii kwa wote) ni sura  moja tu ya Ujamaa.  Lakini pia kuna sura ya pili ambayo ni ya kuuchuma huo utajiri wenyewe wa kugawana.  Katika Azimio la Arusha, unafafanuliwa utaratibu wa kuchuma utajiri bila ya kunyonyana.  Mkakati uliowekwa ni wa njia kuu za uchumi wa nchi kuwekwa chini ya wakulima na wafanyakazi kupitia vyombo vya Serikali

 

Siasa ya Kujitegemea:

 

Siasa ya Kujitegemea imechambuliwa kwa kina katika Sehemu ya Tatu ya Azimio la Arusha.  Siasa hii inajikita katika kuleta maendeleo ya kweli ya nchi na ya wananchi wenyewe hasa wanyonge.  Hoja inajengwa  kwamba huwezi kuzungumzia maendeleo ya kweli kama maendeleo hayo ni ya vitu tu na si ya watu wenyewe na kama maendeleo hayo yamejengwa juu ya msingi wa utegemezi wa fadhila za nje.  Inasisitizwa kwamba fedha si msingi wa maendeleo bali ni matokeo ya maendeleo.  Kwa hivyo mkakati unaotiliwa mkazo ni wa kujituma katika kujiletea maendeleo bila ya kusubiri fedha kwanza au misaada na mikopo kutoka nje.  Vitu hivyo kama vitapatikana vije tu kusaidia juhudi zetu za kujitegemea na kamwe visiruhusiwe kuhatarisha uhuru wetu.

 

Kwa mnasaba huo, Siasa ya Kujitegemea inasisitiza kwamba: maendeleo ya nchi huletwa na watu, hayaletwi na fedha.  Fedha ni matokeo siyo msingi wa maendeleo.  Ili tuendelee twahitaji vitu vinne: (i) Watu; (ii) Ardhi; (iii) Siasa safi na (iv) Uongozi bora. Kwa kuzingatia ukweli kwamba nchi yetu ina watu wengi na eneo kubwa la ardhi, mkakati wa siasa ya kujitegemea unabainisha kwamba maendeleo yataletwa na kilimo na hivyo pia unamjali zaidi mkulima vijijini.

 

Siasa ya Kujitegemea imebainisha masharti mawili ya maendeleo.  Masharti hayo ni Juhudi na MaarifaJuhudi inaashiria kufanya kazi kwa kujituma na Maarifa ni kiashirio cha matumizi ya utaalamu na teknolojia kwa lengo la kuziongezea tija juhudi.

 

Kwa jumla, mtu hahitaji utafiti wa kina kubaini kwamba karibu yote yaliyoelezewa kuhusiana na Siasa ya Kujitegemea yalikuwa na ukweli mwaka 1967 na bado yana ukweli hadi leo.  Aidha, yote hayo yanaendelea kupendwa na Watanzania  waliowengi ambao siyo tu wameyakubali, bali pia wanajitahidi kuyatekeleza.  Kwa mfano Watanzania pamoja na unyonge wao, hawakubali kuonewa wala kunyanyaswa.  Pia, Watanzania wamejiletea maendeleo mengi (shule, zahanati, visima, njia, maji n.k.) kwa kujitegemea bila ya kusubiri fedha.  Na zaidi ya yote, Watanzania wanajituma kwa bidii kubwa.  Kwa kuzingatia ukweli huo, mtu hapaswi kupata taabu sana kuelewa kwa nini Siasa ya Kujitegemea inaendelea kuwa siasa ya CCM.

 

Kama ilivyo katika siasa ya ujamaa, bila shaka yamejitokeza hapa na pale matatizo ya kiutekelezaji.  Yapo matatizo yaliyo nje ya uwezo wetu kamavile matatizo ya kiuchumi ya dunia ambayo yalipotukumba na sisi yaliathiri utekelezaji wetu.  Lakini pia yapo matatizo yaliyotokana na kasoro zetu wenyewe kama vile kuweka mkazo mdogo katika maarifa na badala yake kukazania tu juhudi ambapo matokeo yake  yamekuwa ni tija ndogo katika uzalishaji hasa katika kilimo.  Maeneo kama haya ya matatizo na kasoro ndiyo yanayotoa fursa ya kuzipitia upya baadhi ya sera za Chama kamatutakavyobainisha baadaye.

 

BAADHI YA MAENEO YALIYOHITAJI MAREKEBISHO YA SERA

 

Katika makala haya tumedhihirisha kwa uhakika na bila ya kigugumizi kwamba Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea ndiyo siasa ya CCM na tumelitambua Azimio la Arusha kuwa ndiyo dira kuu inayoongoza uandaaji wa sera za utekelezaji wa siasa hiyo.  Baadhi ya watu wasioitakia mema CCM wamekuwa wakiihukumu siasa hiyo kwa vigezo visivyokuwa sahihi, na ndio waliochangia kwa sehemu kubwa katika kuwababaisha wanachama na viongozi wa CCM.  Watu kama hao wamekuwa wakiitangaza siasa hiyo kuwa iliyoshindwa na kwamba sasa ubepari ndio umejikita.  Kigezo wanachotumia ni sifa za nchi yenye ujamaa kamili zilizotajwa katika Azimio la Arusha kama vile kutokuwapo ubepari wala ukabaila wala matabaka ya watu.  Lakini Azimio la Arusha lenyewe linasema kwamba: Nchi yetu ni nchi ya Wakulima na Wafanyakazi, lakini si nchi ya Ujamaa kamili.  Ina misingi ya ubepari na ukabaila na vishawishi vyake.  Misingi hii ya ubepari na ukabaila yaweza ikapanuka na kuenea.

 

Kwa hivyo, usahihi wa mambo ni kwamba Ujamaa na Kujitegemea ni lengo la muda mrefu ambalo kulifikia kutachukua miaka mingi sana.  Na kwa sababu ubepari na ukabaila upo na utaendelea na jitihada za kujipanua na kujieneza, njia ya kufikia lengo hilo la Ujamaa na Kujitegemea si nyoofu bali ina mipindo, milima na mabonde.  Ni kwa kutambua ukweli huu mchungu ndiyo maana CCM ikajiwekea utamaduni wa kuzipitia upya sera zake kila baada ya muda ili kubaini vikwazo vinavyojitokeza na kujiwekea njia za kuvikwepa.

 

Hapa tutazungumzia mifano mitatu tu ya maeneo ambayo kutokana na kubadilika kwa mazingira na mahitaji ya wakati, CCM ilibidi izifanyie marekebisho sera zake za msingi.  Maeneo hayo yanahusu udhibiti wa njia kuu za uchumi, mazingatio ya maarifa katika kujenga msingi wa  kujitegemea na suala la masharti au miiko ya uanachama.  Ni maeneo haya hasa ndiyo yanayojengewa hoja na wapinzani wetu kwamba CCM imeachana na Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.

 

Udhibiti wa Njia Kuu za Uchumi

 

Kama ilivyokwishagusiwa, Azimio la Arusha lilielekeza kwamba njia zote kuu za uchumi wa nchi zimilikiwe na kutawaliwa na Serikali kwa niaba ya wakulima na wafanyakazi ili faida yote ya harakati za kiuchumi iingie Serikalini ambako itatumika kusambaza huduma mbali mbali za kijamii kwa wananchi, badala ya kuingia mifukoni mwa mabepari na makabaila wachache.  Hata hivyo, utekelezaji wa azma hii njema ulikumbana na matatizo mbali mbali.  Tatizo la kwanza ni kwamba ari ya utekelezaji ilipitiliza mipaka iliyotarajiwa na Azimio la Arusha.  Serikali badala ya kutaifisha njia kuu tu za uchumi, ilitaifisha hata njia ndogo kama vile biashara za reja reja za bidhaa ndogo ndogo zikiwemo hata sindano, bizari, sabuni n.k.  Kujiingiza kwa Serikali katika biashara ndogo ndogo kama hizo kulisababisha upungufu mkubwa wa bidhaa hizo nchini ambapo Tanzania iligeuka kuwa nchi ya foleni za kuzigombania.  Utaratibu huu ukawa umeleta usumbufu mkubwa kwa wananchi, haidhuru hivi sasa baadhi ya watu wameusahau usumbufu huo na kauli mbiu kuu ya wakati huo ya “kufunga mikanda”.

 

Tatizo la pili lilihusu utaifishaji wa hata hizo njia kuu za uchumi zilizotakiwa na Azimio la Arusha.  Baada ya muda wa utaifishaji, mashirika ya umma na viwanda vingi vilijikuta vinapungukiwa na tija kutokana na ubadhirifu, uajiri uliozidi mahitaji na ufinyu wa mitaji.  Njia kuu hizo za uchumi zikawa zinaingiza hasara Serikalini badala ya faida.  Serikali ikajikuta inatumia fedha nyingi kufidia mashirika na viwanda hivyo badala ya kugharamia huduma za kijamii kwa wananchi kama ilivyotarajiwa.  Matokeo yake ni kwamba siyo tu uchumi wa nchi ulidumaa, bali na huduma za jamii ambazo zilikwishapanuka kwa kiasi kikubwa, zilivurugika.  Ikadhihirika wazi wazi kwamba mkakati huu wa kuchuma utajiri wa nchi na kuusambaza kwa wananchi  kwa usawa ulikuwa haufanyi kazi.

 

Kama hayo hayatoshi, kipindi hicho cha mwishoni mwa miaka ya themanini  kilishuhudia upepo mkubwa wa mageuzi ya kisiasa na kiuchumi uliozikumba nchi za kijamaa ambapo madola makubwa makubwa ya Ulaya Mashariki, ikiwemo Urusi ya Kisovieti, yalikuwa yakiporomoka moja baada ya jingine.  Mageuzi hayo yalikuwa ni ya kuleta mfumo wa uchumi wa soko na mfumo wa vyama vingi vya siasa.

 

Katika mazingira hayo, CCM ilibidi kuzitathmini sera zake ili kujiridhisha kama kweli zingeivusha katika matatizo hayo yaliyojitokeza kwenye safari yake ya kuelekea Ujamaa na Kujitegemea.  CCM iliridhika kwamba kama sera hizo zikiachiwa ziendelee kama zilivyo, zingeweza kuua kabisa dhamira ya kujenga ujamaa kama ilivyokuwa imetokea kwa nchi za  Ulaya Mashariki.  Ikabidi itumie kanuni ya mwanzi ambao unapopigwa na upepo mkali, hupinda ukainama hadi kukaribia kugusa chini, lakini upepo ukitulia, mwanzi unasimama tena.  Nchi za Ulaya Mashariki hazikutaka kuinama bali zikabaki na ukakamavu wa mbuyu ambao kwa kushindana kwake na upepo mkali, huweza kujikuta umeanguka kwa kishindo.  Kwa ufupi, mazingira ya kujenga ujamaa yalikuwa yamebadilika.  Kwa hivyo, na mbinu za kujenga ujamaa huo nazo zilipaswa kubadilika.

 

Katika kuelekeza njia ya kuondokana na matatizo yaliyojitokeza kuhusiana na zoezi la kuimilikisha Serikali njia kuu za uchumi, Mwalimu Nyerere alisema yafuatayo katika “Kujitawala ni Kujitegemea” mwaka 1987”.

 

Lakini Azimio halikutaja mpango wa kuonyesha ni shughuli gani imilikiwe na Taifa zima, ni sehemu gani imilikiwe na Serikali za Mitaa, na sehemu gani ishikwe na Vyama vya Ushirika.  Wala Azimio halikusema  ni sehemu gani inaweza kudhibitiwa kwa njia nyingine isiyokuwa ya kumiliki.  Kadhalika Azimio linasema kwamba ardhi lazima imilikiwe na umma; lakini halisemi “shamba lile la eka 100 mali ya Fulani lazima litaifishwe; au shamba lile la eka 99 mali ya Fulani Mwingine lisitaifishwe.”  Mambo kama hayo Azimio limeiachia Serikali, chini ya uongozi wa jumla wa Chama, kupanga yanayofaa ili kutekeleza msingi wa kumiliki na kudhibiti shughuli za umma, kwa kuzingatia mazingira yaliyoko wakati huo.

 

Kwa hiyo tunapopata tatizo jipya, tunajadili tena na kuamua sehemu gani ya shughuli ishikwe na umma, na shughuli gani za uchumi katika nchi yetu zinaweza kudhibitiwa kwa njia nyingine kama leseni, kodi au utaratibu mwingine.

 

Ilikuwa ni katika mazingatio hayo ndiyo Mwelekeo wa Sera za CCM Katika Miaka ya Tisini ulipotungwa.  Mwelekeo huo unaelezewa kwa majumuisho na kifungu cha 1 (Sura ya Tatu) cha “Ilani ya Uchaguzi ya CCM, Uchaguzi Mkuu, Oktoba 1955” kama ifuatavyo:-

 

 1. Ujamaa na Kujitegemea:

 

Katika kuendeleza kuufufua na kuujenga uchumi wa Taifa Serikali ya CCM itaongozwa na Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea inayolingana na wakati tulionao.

 

Shabaha ya Ujamaa katika kipindi hiki, ni kuwafanya wananchi wenyewe kuwa ndio wamilikaji wakuu wa uchumi, na dola kuwa zaidi mhimili wa uchumi wa Taifa.  Kwa mantiki hiyo, wananchi wamiliki uchumi wa kilimo, ufugaji, uvuvi, viwanda, madini nakadhalika, moja kwa moja kila mtu binafsi, wamiliki kwa vikundi vya ushirika wa aina mbali mbali, wamiliki kwa kununua hisa katika makampuni ya wananchi au kununua hisa katika makampuni ya ubia.

 

 

 

 

 

Kimsingi mabadiliko hayo hayakuugusa msingi wa Azimio la Arusha wa uchumi kumilikiwa na wananchi.  Kilichobadilishwa ni msisitizo wa umilikaji huo kufanywa na Serikali kwa niaba ya wananchi, na badala yake sasa unatakiwa ufanywe na wananchi wenyewe moja kwa moja kwa njia mbali mbali.  Uamuzi huo una dhamira ya kuwaongezea wananchi uwezo wa kumiliki uchumi wa nchi yao.

 

Mabadiliko hayo ndiyo msingi wa sera ya uchumi wa soko ambapo sekta ya binafsi imetambuliwa na kupewa fursa ya kushiriki katika kukuza uchumi (kujenga utajiri wa nchi).  Mabadiliko hayo pia ndio msingi wa sera ya ubinafsishaji ambayo si mada ya makala haya.

 

Ni kweli uchumi wa soko na ubinafsishaji ni miongoni mwa viashiria vya ubepari.  Lakini ni kweli pia kwamba uzoefu ulimwenguni kote unaonyesha kwamba njia hizo za kujenga uchumi zina ufanisi mkubwa katika kukuza uchumi.  Ujamaa una malengo makubwa sana ambayo yanahitaji uchumi imara kuweza kuyafikia.  Ndiyo maana Karl Marx, mwasisi wa falsafa ya ujamaa wa kisayansi, aliamini kwamba nchi haiwezi kujenga Ujamaa kamahaikupitia kwanza hatua ya ubepari uliopea.  Naye Deng Hsiao Ping aliyeleta mageuzi makubwa ya ujenzi wa Ujamaa nchini China baada ya Mao Dze Tung katika miaka ya sabini alipoulizwa kama sera zake zilizoonekana kutumia ubepari zilikuwa zinaitoa China katika ujenzi wa Ujamaa, alijibu kwa ufupi tu kwamba walikuwa wanatumia ubepari kujenga ujamaa.

 

Kwa hivyo, hata kwa CCM, “Mwelekeo wa Sera za CCM Katika Miaka ya Tisini” na baadaye “Mwelekeo wa Sera za CCM Katika Miaka ya 2000-2010” ni mkakati mpya wa Chama wa kujenga uwezo wa kiuchumi utakaohimili mahitaji ya malengo ya Ujamaa.

 

Lakini pia ingefaa ieleweke kwamba ingawa Serikali imepunguziwa kwa kiasi kikubwa jukumu la umiliki wa njia kuu za uchumi, lakini bado imeachiwa jukumu la kuutawala au kuudhibiti uchumi kwani kama ilivyokwishaonyeshwa, Serikali inabaki kuwa mhimili wa uchumi.  Katika kutekeleza jukumu hilo la mhimili, Serikali inatarajiwa kusimamia na kufuatilia kwa karibu shughuli za kiuchumi za wananchi na kuzitungia sheria, kanuni na taratibu zitakazohakikisha kwamba makali ya ubepari yanadhibitiwa na kwamba lengo la kujenga Ujamaa halipotezwi.

 

Tunapenda kusisitiza kwamba mabadiliko haya hayakufanywa kwa kubahatisha bali yalizingatia kwa ukamilifu mambo ya msingi ya Azimio la Arusha na maelekezo ya Baba wa Taifa.  Wapo baadhi ya wanasiasa na wasomi wanaoitaka CCM itangaze kwamba sasa inajenga ubepari nchini, eti kwa sababu tu ya kuwapo nchini kwa viashiria vya ubepari.  Wanasema hayo wakijua kwamba nchi za kibepari zimekwa kwa muda mrefu sasa zikitumia mazuri ya Ujamaa kupunguza makali ya ubepari.  Mazuri hayo ni pamoja na kutoa fursa sawa za elimu na huduma nyingine za jamii, kuboresha maslahi na mazingira ya kazi kwa wafanyakazi (tofauti na yale aliyoyashuhudia Karl Marx wakati akiandika nadharia yake ya ujamaa wa kisayansi) na kuwatoza kodi kubwa kubwa matajiri ili Serikali ipate fedha za kuwahudumia maskini.  Mataifa ya kibepari yanapochukua hatua kama hizo ambazo kimsingi ni za kijamaa, hayajiiti ya kijamaa, hayasemi yanajenga Ujamaa na wala hayana lengo la kujenga Ujamaa.  Kwa nini CCM inapopanga mkakati wa kuyatumia yale ya kibepari yanayoweza kusaidia kujenga Ujamaa ilazimishwe kujitangaza kuwa sasa ni Chama cha kibepari au kinachojenga ubepari?  Wanaoitaka CCM itangaze  kuwa inajenga ubepari wana agenda ya siri ya kutaka CCM ikose imani ya Watanzania na wao wapate mwanya wa ubabaishaji wa kujitangaza kuwa wao ndio wajamaa na watetezi wa wanyonge.  Aghlabu ni watu hao hao ambao hivi sasa eti wanajinasibisha na Baba wa Taifa lakini wakati alipokuwa Mkuu wa Nchi na Chama akiongoza ujenzi wa Ujamaa katika mazingira ya wakati ule, wakimlaumu na kumkosoa hata kama ni kwa siri.  Kama si wanafiki ni nani?

 

 

 

 

 

 

Mazingatio ya Maarifa Katika Kujenga Msingi wa Kujitegemea:

 

Tumekwishaeleza kwamba Azimio la Arusha limeyataja juhudi na maarifa kuwa ndiyo masharti ya maendeleo.  Tumeeleza vile vile kwamba uzoefu unaonyesha kwamba Watanzania wamekuwa wakitumia zaidi juhudi kuliko maarifa, hasa katika kilimo na hivyo uzalishaji wa mali haujawa na tija ya kutosha.  Matokeo yake ni kwamba uchumi wa nchi umeendelea kuwa ulio nyuma na tegemezi.  Lakini tumekwishaonyesha pia kwamba malengo ya Ujamaa ni makubwa na kamwe hayatoweza kufikiwa kama uchumi wa nchi utaendelea kuwa wa namna hii.

 

Ni katika mazingatio ya ukweli huu ndiyo “Mwelekeo wa Sera za CCM Katika Miaka ya 2000 Hadi 2010” ulipotungwa.  Mwelekeo huu wa sera umetoa msisitizo kwenye kujenga msingi wa uchumi wa kisasa wa taifa linalojitegemea na kutumia mkakati wa “modenaizesheni”, yaani matumizi ya teknolojia ya kisasa katika kilimo, ufugaji, uvuvi, viwanda n.k. ili kukuza tija na hivyo utajiri wa nchi.

 

Sura ya Pili ya Mwelekeo huu wa sera inalichambua kwa kina suala hili.  Itoshe tu hapa kunukuu ibara za 19 na 20 za Mwelekeo kama ifuatavyo:-

 

 1. Uzoefu wa dunia unaonyesha kuwa huduma za kiuchumi na za kijamii za kisasa; barabara, mahakama, elimu, afya, maji n.k. zote zinagharamiwa na uchumi wa kisasa. Hivi ndivyo ilivyo Ulaya, Marekani n.k. na hakuna mgongano.  Nchi za Asia ambazo mara  nyingi tunazitolea mifano zimeelewa hilo na wamechukua na wanaendelea kuchukua hatua za kuufanya uchumi wao uwe wa kisasa zaidi ili umudu kubeba gharama za huduma za jamii, mahakama, barabara n.k. kutokana na misaada na mikopo kutoka kwa wahisani.  Hili si jawabu la kudumu.  Jawabu la kudumu ni kujenga nguvu za uchumi wetu za kulipia gharama hizo za lazima za maendeleo yetu.

 

 

 1. Katika azma ya kujenga msingi wa uchumi wa kisasa (Modenaizesheni) wa taifa linalojitegemea msukumo wetu uelekezwe kwenye maeneo yafuatayo (ambayo yamebainishwa na kuchambuliwa.  Maeneo hayo ni elimu ya kisasa; kilimo, ufugaji na uvuvi wa kisasa; viwanda; madini; utalii; miundombinu ya kiuchumi; sera muafaka za fedha na biashara; na kazi, maarifa, nidhamu, idadi ya watu na maendeleo ya uchumi.

 

Nayo kwa upande wake, “Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2000” inafanya majumuisho kama ifuatavyo katika ibara yake ya pili:-

 

 1. Mwelekeo wa Sera za CCM za Miaka ya 2000 hadi 2010 unaunganisha malengo makuu haya ya Mwelekeo wa Sera za CCM Katika Miaka ya Tisini na kuendeleza utekelezaji wake ili kujenga msingi wa uchumi wa kisasa wa Taifa linalojitegemea na uwezeshaji wa kiuchumi wa wananchi. Uchumi wa sasa wa Tanzania ni uchumi ulio nyuma na tegemezi.  Nchi haiwezi kujitegemea kiuchumi wakati uchumi wake uko nyuma na pia uchumi wake hauwezi kuwa ulioendelea kama haujitegemei.  Kadri uchumi unavyozidi kuwa wa kisasa, yaani modenaizesheniya uchumi wa taifa, ndivyo nchi inavyoingia katika mkondo wa kujitegemea kiuchumi …  Uchumi wa kisasa utajengwa kwa kuhakikisha kuwa sayansi na teknolojia ya kisasa inapenyezwa katika sekta zote ili hatimaye kuutokomeza umaskini nchini.”

 

Katika juhudi hizo zinazofanywa na CCM za kujenga msingi wa uchumi wa Taifa linalojitegemea katika mazingira ya utandawazi unaosukumwa na ubepari, tunahitaji mitaji mikubwa na teknolojia ya kisasa.  Walionazo nyenzo hizo za msingi kwa sasa ni mabepari.  Kwa hivyo hakuwezi kuwa na njia ya mkato katika kuzipata nyenzo hizo ila kuwakaribisha kama wawekezaji.  Hiyo ndiyo mantiki ya sera za ubinafsishaji na kuvutia vitega uchumi hata vya nje, nchini.  Lakini katika kuwalinda wanyonge na kuwawezesha nao kuhimili ushindani, ndiyo maana CCM imeweka mkakati wa kuwawezesha wananchi, ambao ni mada iliyo nje ya upeo wa madhumuni ya makala haya.

 

 

 

Masharti/Miiko ya Uanachama:

 

Sehemu ya Tano ya Azimio la Arusha inaweka masharti sita yafuatayo kwa viongozi:

 

 1. Kiongozi wa TANU (baadaye CCM) au wa Serikali sharti awe mkulima au mfanyakazi na asishiriki katika jambo lo lote la kibepari au kikabaila.
 2. Asiwe na hisa katika makampuni yo yote.
 3. Asiwe mkurugenzi katika kampuni ya kikabaila au kibepari.
 4. Asiwe na mishahara miwili au zaidi.
 5. Asiwe na nyumba ya kupangisha.
 6. Viongozi tunaofikiria hapa ni wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Mawaziri, Wabunge, Wakuu wa Vyama vilivyoshirikishwa na TANU (baadaye Jumuiya za CCM), Wakuu wa Mashirika ya Kiserikali, Viongozi kutokana na kifungu cho chote cha Katiba ya TANU (baadaye ya CCM), Madiwani, na Watumishi wa Serikali wenye vyeo vya kati na vya juu. (Kwa mujibu wa kifungu hiki kiongozi ni mtu na mkewe au mke na mumewe).

 

Lengo la msingi la masharti haya lilikuwa ni kujenga maadili mema ili miongoni mwa viongozi wasitumie madaraka yao kujinufaisha binafsi.

 

Hata hivyo, kufuatia “Mwongozo wa 1981”, masharti hayo ya uongozi yakafanywa ya wanachama wote na kuingizwa kwa namna hiyo katika Katiba ya CCM ya 1982.  Utekelezaji wa masharti haya ulifikia hatua ya kuwafukuza watu uanachama hata kwa sababu ya kufuga kuku 500 tu au kupangisha vibanda vyao.  Hali hiyo ilitoa picha kama kwamba ujamaa ni umaskini na kwamba kila ukiwa maskini zaidi ndiyo unakuwa  mjamaa zaidi.  Watu wakaogopa kufanya shughuli za kuchuma mali hata zile za halali.   Ubunifu wa kujikwamua na umaskini ukavia katika jamii.  Hili siyo lengo la Ujamaa.

 

Ujio wa mabadiliko makubwa ya kiuchumi, kijamii na kisiasa katika miaka ya tisini kuliifanya CCM iitazame upya mikakati yake ya kujenga Ujamaa.  Kwanza iliona ina wajibu wa kuwaondoa Watanzania katika utamaduni wa kuthamini umaskini uliokuwa unaanza kujengeka kwa jina la Ujamaa na Azimio la Arusha.  Pili, katika mazingira ya mfumo wa vyama vingi, haikuona uhalali wa kuendelea kuwafunga mikono wanachama wa CCM tu na kuwaacha wengine wafaidike peke yao na mageuzi ya kiuchumi yaliyokuwa yanaandaliwa.

 

Ni kwa msingi na mazingatio hayo na mengineyo ndipo CCM katika Maamuzi ya Zanzibar ya 1991 (ambayo huitwa Azimio la Zanzibar kwa makosa na baadhi ya watu) ilipopitisha maamuzi ya msingi yafuatayo:-

 

(1)            Masharti ya uanachama yarejeshwe kuwa ya viongozi tu kama ilivyokusudiwa katika Azimio la Arusha.

(2)            Msisitizo wa masharti ubaki katika kuhakikisha maadili mema miongoni mwa viongozi na kuwaongezea uwajibikaji kama ilivyokusudiwa katika Azimio la Arusha badala ya kuwazuwia kushiriki katika shughuli halali za kujipatia riziki.

(3)            Zaidi ya wakulima na wafanyakazi, wananchi wengine wenye kufanya shughuli nyingine halali za kujipatia riziki (wakiwemo wafanyabiashara) waruhusiwe kujiunga na CCM.

 

Katika eneo hili pamekuwa na upotoshaji makubwa kwamba eti viongozi wameondolewa masharti na miiko na kwamba kwa hivyo eti, Maamuzi ya Zanzibar yalikiuka Azimio la Arusha.  Hii si sahihi hata kidogo.  Viongozi bado wanafungika na masharti ya msingi ya Azimio la Arusha.  Na katika kuhakikisha hivyo, ibara ya 17 ya Katiba ya CCM (toleo la 1997) inataja sifa za Kiongozi na ibara ya 18 imeiweka bayana miiko ya Kiongozi.  Tunazinukuu hapa chini ibara hizo ili kuondoa shaka:-

 

 1. Pamoja na kutimiza masharti ya Uanachama kama  yalivyoelezwa katika Katiba, Kiongozi sharti pia awe na sifa zifuatazo:-

               

(1)            Awe ni mtu aliyetosheka, na asiwe mtu aliyetawaliwa na tamaa.

(2)            Awe ni mtu anayependa kueneza matunda ya uhuru kwa wananchi wote kwa ajili ya manufaa yao na maendeleo ya Taifa kwa jumla.

 

 1. (1) Ni mwiko kwa kiongozi kutumia madaraka aliyopewa ama

kwa ajili ya manufaa yake binafsi au kwa upendeleo, au kwa namna yoyote ambayo ni kinyume cha lengo lililokusudiwa madaraka hayo.

(2)            Ni mwiko kwa kiongozi kupokea mapato ya kificho, kutoa au kupokea rushwa au kushiriki katika mambo yoyote ya magendo au mambo mengine ambayo ni kinyume cha lengo lililokusudiwa madaraka hayo.

 

Miiko hii inalinda misingi ya masharti ya uongozi ya Azimio la Arusha na kamwe haipingani nayo wala kuidhoofisha au kuifuta kama inavyodaiwa na baadhi ya wanasiasa na wasomi.

 

HITIMISHO:

 

Tumeonyesha katika makala haya kwamba CCM haijaachana kamwe na Ujamaa na Kujitegemea.  Ujamaa na kujitegemea ndiyo siasa au itikadi ya CCM.  Ujamaa na Kujitegemea ndilo lengo la msingi na la kudumu la CCM.  Kwa CCM, lengo hilo halibadiliki.  Tunaamini hivyo hata kwa nchi kwani Watanzania wanapenda Ujamaa na wanachukizwa na ubepari.

 

Tumeonyesha pia kwamba Azimio la Arusha linaendelea kuwa dira ya CCM katika safari ndefu na ngumu ya kujenga Ujamaa na Kujitegemea.  Kwa hivyo, wale wanaodai kuwa CCM haina dira ama hawajaelewa, au ni wababishaji tu au mbaya zaidi, ni wapotoshaji wa makusudi wenye agenda ya siri ya kuipaka matope CCM kwa lengo la kujinufaisha kisiasa.  Azimio siyo tu ni dira, bali ndilo chimbuko la sera mbali mbali za CCM za utekelezaji wa siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.  Mara chache sana Azimio huweza kubadilika na wakati kwa vipengele visivyokuwa vya msingi, bila ya kuathiri lengo na madhumuni ya msingi.  Mabadiliko ya aina hiyo yaliridhiwa hata na Baba wa Taifa mwenyewe.  Na ndiyo maana alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza walionunua hisa za Benki ya CRDB ilipobinafsishwa.

 

Aidha tumeonyesha katika makala kwamba kinachobadilika kila baada ya muda ni sera na mikakati ya utekelezaji wa Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.  Sera hutungwa kwa ajili ya kutoa mwelekeo katika jambo mahsusi kwa kipindi fulani, ndani ya upeo wa dira kuu (Azimio la Arusha) na kwa kulenga lengo kuu (Ujamaa na Kujitegemea).  Vivyo hivyo kwa mikakati ya utekelezaji wa sera hizo.

 

Pia, katika makala haya, tumekiri kama linavyokiri Azimio la Arusha lenyewe kwamba Tanzania si nchi ya ujama kamili.  Na wala haijawahi hata siku moja kuwa nchi ya ujamaa kamili.  Lakini chini ya CCM, Ujamaa na Kujitegemea ndilo lengo kuu ambalo kulifikia kwake si kazi rahisi wala ya muda mfupi.

 

Tumejenga pia hoja kwamba kuwepo kwa viashiria vya ubepari nchini (ambavyo vimekuwapo toka enzi za ukoloni na wakati Azimio linaandikwa na baadaye kutekelezwa) haiwezi ikawa sababu ya kuitaka CCM itangaze kuwa inajenga ubepari kama baadhi ya wanasiasa na wasomi wanavyotaka.  CCM inayatumia yale ya ubepari yanayoweza kusaidia katika ujenzi wa Ujamaa, kama vile yanavyofanya mataifa ya  kibepari ambayo yamefanikiwa kuyatumia mazuri ya Ujamaa katika kupunguza makali ya ubepari.  Kwa hivyo, CCM kwa mazingira ya wakati huu, kutumia sera za uchumi wa soko na ubinafsishaji kisiwe kioja.

 

CCM inajua inachokifanya kama ibara ya 9 ya”Ilani ya Uchaguzi Oktoba, 2000” inavyobainisha;  yaani:-

 

 1. Chama Cha Mapinduzi kinasimamia utekelezaji wa mageuzi ya kisiasa na kiuchumi huku kikielewa kwamba katika kipindi cha awali cha utekelezaji wake, uchumi wa soko huwanufaisha walionacho na wajanja wachache.  Kwa msingi huo Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kuchukua hatua madhubuti za kisera ili kuwalinda na kuwawezesha kiuchumi wanaoathirika na ushindani na uchumi wa soko.  Lengo ni kutekeleza uchumi wa soko na wakati  huo huo kuelekeza faida na ziada zitokanazo na sekta za umma na binafsi katika kupambana na umaskini.

 

                    Matokeo ya hatua hizo yatachukua muda kuonekana na hivyo si sahihi kuzihukumu hivi sasa, kiasi cha miaka kumi tu toka zianze kuchukuliwa, kama baadhi ya wanasiasa na wasomi wanavyofanya bila ya kupendekeza hatua mbadala.

 

Tumeonyesha pia katika makala haya kwamba kubwa lililofanywa na Maamuzi ya Zanzibar ni kuwaondolea wanachama wa CCM mzigo wa masharti ya uongozi na badala yake kuyaacha kwa viongozi wenyewe tu kama ilivyokusudiwa na Azimio la Arusha.  Kwa hivyo, madai kwamba Maazimio ya Zanzibar yamelidhoofisha au kuliua Azimio la Arusha si sahihi na ni upotoshaji mtupu.

 

Tunamalizia kwa kusisitiza kwamba mabadiliko ya sera hayafanywi kwa kukurupuka tu.  Yanafanywa kwa uangalifu mkubwa kwa kuhakikisha kwamba juhudi za kujenga Ujamaa hazivurugiki na lengo halipotezwi.  Azimio la Arusha lenyewe limeacha wazi milango ya mabadiliko na Baba wa Taifa mwenyewe aliridhia uwezekano huo mwaka 1987 katika hotuba yake maarufu ya “Kujitawala ni Kujitegemea”.