UHURU

UHURU 20.09.2005

 • CUF yadaiwa kupanga mbinu kupinga matokeo
 • Mkapa aiambia TRA  sh. bilioni 150 kwa mwezi hazitoshi
 • Magoba: CUF imejaa chuki, ubinafsi, fitina na majungu
 • Kikwete asema ajira kuongezwa maradufu
 • ‘Wapinzani wanagombania ruzuku kwa maslahi binafsi’
 • Kampeni za Hawa Ghasia zasababisha matawi ya wapinzani kufungwa
 • Hifadhi ya Wamimbiki yatoa milioni nne kusaidia ukarabati za zahanati
 • FGG yatoa sh. Milioni 139 kuboresha mazingira Tabora
 • Mwenegoha aahidi kuendeleza huduma ya uji shuleni na hospitali

CUF yadaiwa kupanga mbinu kupinga matokeo

 • Yaandaa vijana kufanya vurugu kubwa nchini
 • Chaandalia usafiri watu wakapige kura Zanzibar

Na Mwandishi Wetu

CHAMA cha CUF kinadaiwa kuandaa mikakati ikiwemo ya kupinga matokeo ya kushindwa wagombea wa udiwani, ubunge na Rais kupitia chama hicho baada ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 30, mwaka huu.

Habari zilizopatikana zimesema Chama hicho pia kimeandaa usafiri maalum wa boti ambazo zitafanya kazi ya kuwasafirisha wanachama wake wanaoishi Bara kwenda kupiga kura Zanzibar na baadaye kurudi Bara kuja kupiga kura.

Wanaotarajiwa kusafirishwa siku hiyo wanadaiwa kujiandikisha Bara na Zanzibar kwa kutumia majina tofauti na kwamba mpango huo umegundulika baada ya mmoja wao kukutwa na vitambulisho viwili vya mpiga kura vyenye picha yake, lakini vikiwa na majina tofauti.

 

Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF, aliyejitambulisha kwa jina la Mohamed Ngayonga alipoombwa kuzungumzia maandalizi na mikakati hiyo jana alikataa kuongea lolote kwa madai kwamba gazeti la Uhuru limekuwa likiandika vibaya masuala ya CUF.

Uchunguzi zaidi umeonyesha kwamba CUF pia inadaiwa  kuwaapisha wanachama wake wasikubali matokeo ya kushindwa mwaka huu hata kama Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na ile ya Zanzibar (ZEC) zitatangaza kushindwa kwa wagombea wa chama hicho nchini, lakini nguvu zaidi inaelekezwa jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake.

Habari za uhakika zilisema Chama hicho katika kujiimarisha kwa masuala ya mawasiliano, kimeamua kugawa vyombo vya mawasiliano (Radio Call) kwa vijana wake ili kuweza kutimiza azma hiyo.

Tayari baadhi ya vijana wa CUF walioko Manzese walipata redio hizo tangu wiki iliyopita na kwamba hivi sasa wanaendelea kupata mafunzo ya jinsi ya kuwasiliana.

‘Radio Call’ hizo zinadaiwa zitatumika zaidi siku ya kutangaza matokeo ambapo wanachama wa CUF watakuwa wanangoja maelekezo ya mara kwa mara kutoka kwa viongozi wao.

Juzi katika toleo ya Mzalendo, ambalo ni gazeti ndugu na hili lilimkariri Mwenyekiti wa Taasisi ya  Khidmat Daawat  Islamiya (Watumishi waongeaji wa neno la Mungu), Sheikh Shaaban Magezi akisema CUF ina mpango wa kufanya vurugu mara baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa.

Sheikh Magezi alisema kwa bahati mbaya zaidi, CUF inashirikiana kwa karibu na Shura ya Maimam ambao wana historia ya kuendesha vitendo vya vurugu, likiwemo tukio la Msikiti wa Mwembechai.

Alisema Shura ya Maimam inaunga mkono kazi gaidi namba moja duniani, Osama Bin Laden duniani na kwamba iliwahi kuchangisha fedha kwa nia ya kumsaidia ‘huko’ aliko.

 

 

 

Mkapa aiambia TRA  sh. bilioni 150 kwa mwezi hazitoshi

 • Ataka Wafanyakazi wasibweteke, waongeze juhudi
 • Asema  serikali ya awamu ya nne inawategemea sana

Na Mwandishi Wetu

RAIS Benjamin Mkapa amehimiza wafanyakazi wa Mamlaka ya Kodi nchini (TRA) kutobweteka na mafanikio ya ukusanyaji wa kodi hadi kufikia kiasi cha sh. bilioni 150 kila mwezi kwa sasa.

Aidha, Rais Mkapa amewataka wafanyakazi hao kuongeza kasi ili waweze kuchangia pato la taifa kwa asilimia kubwa zaidi kuliko ilivyo sasa.

Mkapa alitoa rai hilo jana alipozungumza na wafanyakazi wa TRA baada ya kutembelea ofisi zao pamoja na maeneo ya Bandari kujionea mitambo ya kupima mafuta yanayoingia nchini.

Alisema pamoja na mafanikio ya kuongeza makusanyo kutoka sh. bilioni 25 kwa mwezi mwaka 1995 hadi sh. bilioni 150 Juni, mwaka huu, bado makusanyo hayo yanachangia asilimia 13.8 ya pato la taifa wakati nchi jirani ya Malawi makusanyo yanachangia asilimia 18 na Kenya yanachangia asilimia 20 ya pato la Taifa.

‘’Tumepunguza kidogo utegemezi kwa wahisani, lakini bado matumizi ya serikali yanategemea sana misaada na mikopo kutoka nje,’’ alisema na kuongeza kwamba Serikali ya awamu ya nne itakuwa na kazi ya kuimarisha Uhuru wetu kwa kupunguza utegemezi huo.

Alisema kipindi kijacho ni kipindi cha kupunguza uhasama na walipa kodi ili kuwepo ukusanyaji wa mapato endelevu.

Akizungumzia umuhimu wa kukusanya mapato kwa manufaa ya wananchi, Rais Mkapa alisema suala la kukusanya kodi ni la muhimu zaidi kipindi kijacho ili serikali iweze kutekeleza mpango wake wa Kukuza Uchumi na kupunguza Umasikini (MKUKUTA).

‘’Serikali ya awamu ya nne inakutegemeeni sana, na inatarajia kutoka kwenu mapato zaidi yanayohitajika katika kufanikisha programu zetu zaidi kuliko wakati uliotangulia,’’ alisema.

Rais alisema kitendo cha kuweka mita ya kupima mafuta yanayoingia nchini na mitambo ya kukagua makontena ni moja ya jitihada za makusudi ya kuongeza kasi ya kukusanya mapato, na kwamba pamoja na uzuri wake, TRA itambue kwamba baadhi ya wafanyakazi wake wanaweza kuchukia hatua hiyo jambo ambalo alisema lazima wawe makini.

‘’Lakini kwa vile vitendea kazi kama hivi vya uhakika vinavyoziba mianya ya wakwepa kodi, ni adui wa watumishi wasio waaminifu na watu wanaotaka kukwepa kodi, vitapigwa vita na pengine kuhujumiwa, hivyo muimarishe sana ulinzi wake,’’ alisema.

Alishauri TRA kuangalia mianya mbalimbali ya kuongeza wigo wa kodi za ndani kutokana na ukweli kwamba kodi za nje zinaweza kupungua kutokana na mikataba au makubaliano mbalimbali yaliyofikiwa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuia ya Maendeleo ya Nchi za kusini mwa Afrika (SADC).

Awali, aliwashukuru wafanyakazi wote wa TRA kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya tangu ilipoanzishwa mwaka 1996.

 

 

 

 

Magoba: CUF imejaa chuki, ubinafsi, fitina na majungu

Na Mussa Mahiki

MBUNGE wa zamani wa jimbo la Kigamboni, Frank Magoba, amesema chama cha Civic United Front (CUF) kimejaa chuki, ubinafsi, fitina na majungu.

Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni wa CCM kuwanadi  wagombea wa udiwani na  ubunge uliofanyika juzi kwenye Uwanja wa CCM tawi la Mbagala Rangitatu, Magoba alisema ilikuwa vigumu kutekeleza miradi ya maendeleo kwenye jimbo lake kwa kuwa viongozi wake hawakuwa tayari kutoa ushirikiano.

Katika mkutano huo ambao Magoba alimnadi mgombea udiwani wa CCM Kata ya Charambe, Cecilia Macha na mgombea ubunge wa jimbo la Kigamboni, Msomi Mwinchoum, alisema viongozi waandamizi wa CUF walikuwa na chuki binafsi dhidi yake na wakati mwingine walimjengea majungu ambayo hayakuwa na msingi ili ashindwe kutekeleza majukumu yake kama mbunge.

Mbunge huyo wa zamani alisema ili atekeleze majukumu yake ilimpasa ashirikiane bega kwa bega na watendaji wa serikali ambao wametoka Chama tawala, lakini viongozi wake walikuwa hawapendi kuona hali hiyo inatokea na kuanza kumjengea fitina na kumtenga katika utekelezaji wa majukumu yake.

“Wananchi mmekuwa mnasikia tu kwenye vyombo vya habari kuwa nimetoka CUF na kujiunga na CCM, lakini hamjui sababu zilizonifanya nihame huko na kurudi CCM. CUF kumejaa chuki, ubinafsi, majungu na fitina hizo ndizo sababu zilizonifukuza na kurudi nyumbani,” alisema.

Alisema mahali popote penye majungu kazi haiwezi kufanyika, hivyo ilikuwa vigumu kwake kuendelea kung’ang’ania CUF wakati wananchi wanahitaji huduma muhimu za jamii lakini chama kinashindwa kutekeleza wajibu wake kwa wananchi waliomchagua, hivyo aliamua kurejea CCM.

Magoba ambaye alikuwepo kwenye mchakato wa kumpata mgombea wa ubunge kupitia chama hicho alisema katika miaka michache aliyokuwepo ndani ya vyama vya upinzani amejifunza mambo mengi mabaya na yasiyokuwa ya kistaarabu kama kuhamasisha vijana kufanya fujo na kuvunja amani.

Alisema vitendo vinavyofanywa hivi sasa na vijana ambao ni mashabiki, wapenzi na wanachama wa CUF wa kupita barabarani kwa maandamano na kufanya uporaji wa mali, upigaji watu,  uharibifu wa mali za watu na utoaji wa lugha chafu kwa wagombea wa CCM vinaashiria shari.

Alisema atahakikisha vijana wote wanaofanya vitendo hivyo wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa kuwa vijana hao wanafahamika na mahali wanapoishi panajulikana.

Akizungumza katika mkutano huo mgombea udiwani Cecilia aliwataka wanaCCM kujenga umoja, ushirikiano na mshikamano ili kuweza kurejesha kiti cha udiwani kwenye kata hiyo kwa CCM.

Naye mgombea ubunge Mwinchoum alisema sera na Ilani ya Uchaguzi ya CCM inatekelezeka kwa sababu Chama kina uzoefu na ndicho kikongwe kuliko vingine.

Alisema uzoefu na ujuzi wa viongozi wa CCM ndio utakaowezesha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi na hivyo kuwaletea wananchi maendeleo yaliyokosekana kwenye jimbo hilo kwa muda mrefu.

 

 

Kikwete asema ajira kuongezwa maradufu

Na Bashir Nkoromo, Nkenge

MGOMBEA urais kwa tiketi ya CCM, Jakaya Kikwete, ameahidi iwapo atapata ridhaa ya Watanzania kuongoza nchi, atapanua ajira maradufu katika sekta za afya na elimu.

Alisema Serikali yake inatarajiwa kutoa kipaumbele kwa sekta ya kilimo kama mkombozi wa wananchi kiuchumi, kutokana na kuendeshwa kisasa na yatima kusomeshwa bure.

Kikwete, ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, alisema hayo jana katika mkutano wa kampeni mjini hapa.

Mkutano ulijawa bashasha na umati wa watu kufurika, misafara yake ikiongozwa na pikipiki za wakereketwa alipopita vijijini, alijikuta akisimamishwa mara kwa mara hadi kuchelewesha ratiba, baadhi wakitaka walau wamguse tu.

Alisema ajira hiyo, itatokana na azma ya serikali kuwawekea katika kuendeleza juhudi za serikali ya awamu ya tatu, kwa kujenga shule na vituo vya afya zaidi.

Aliwasihi wananchi kuchagua CCM, kwani sera yake pia imedhihirisha kutekelezeka, tofauti na wapinzani, ambapo alinukuu kauli ya Jaji Joseph Warioba, kuwa ni ‘walalamishi’ tu.

Alitoa mfano wa utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) ulivyofanikiwa kwa kujenga madarasa na kuwa hiyo inadhihirisha ni jinsi CCM inavyojali wananchi wake.

Pia aliwahakikishia wananchi hao kuhusu juhudi za kuendeleza elimu kwa kupanua nafasi hizo kutoka elimu ya msingi hadi vyuo vikuu.

Kwa upande wa uchumi, mgombea huyo aliwaambia wananchi kuwa sekta ya kilimo katika utawala wake itashika nafasi kubwa kama mhimili wa uchumi kitaifa.

Alisema, kupitia mkakati huo, atahakikisha wakulima wanapata mikopo ya kununulia pembejeo na kuendeleza kilimo cha kisasa, kuachana na kile alichokisema “kinategemea damu”.

Pia soko la mazao ikiwemo kahawa inayozalishwa kwa wingi mkoani hapa itaboreshwa.

Kikwete alisema kilimo kikiboreshwa na kuchukua sura ya kisasa kitakomboa wananchi kiuchumi, pia kukidhi matatizo ya makundi maalum ikiwemo vijana na wanawake.

Kuhusu na janga la Ukimwi ambalo limeathiri wananchi wengi mkoani hapa, alisema serikali yake itanedelea kuwajali ikiwa ni pamoja na kuongeza idai ya dawa za kurefusha maisha kwa waathirika na uzazi salama dhidi ya maambukizi hayo.

Kwa mujibu wa Kikwete, dawa hizo za kurefusha maisha kwa waathirika, atahakikisha zinapatikana maradufu kulinganisha na sasa zinavyopatikana kwa watu 40,000 tu.

Pia aliwataka wananchi wa jimboni hapa, ambako ni mpakani na Uganda kuzingatia amani dhidi ya ghiliba ya wasiotakia mema nchi na aliwakumbusha uzoefu wa madhara ya vita vya Kagera.

Katika mikutano hiyo,  Kikwete alifuatana na baadhi ya viongozi akiwemo Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM, Jackson Msome na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera, Pius Ngeze. Wengine ni wagombea ubunge wa CCM, Eustace Katagira (Kyerwa), Dk.Dodorus Kamala (Nkenge) na Nazir Karamagi (Bukoba Vijijini).

Miongoni mwa vijiji alivyotembelea Kikwete na kufanya mikutano yake ya kampeni ni Katoma, Kemondo Bay, Katanga na Kamachumu katika wilaya za Karagwe na Bukoba Vijijini.

 

 

‘Wapinzani wanagombania ruzuku kwa maslahi binafsi’

Na Rodrick Makundi, Moshi

VYAMA vya upinzani nchini vimeelezwa kuwa vinagombania ruzuku kwa manufaa ya wachache katika vyama hivyo na sio kwa ajili ya kuharakisha mipango ya maendeleo kwa wananchi ambao ndio wapiga kura.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na aliyekuwa Mbunge wa Moshi vijijini (TLP), Thomas Ngawaiya, alipokuwa akiwanadi wagombea wa udiwani, ubunge na urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi.

Alikuwa akiwahutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara katika kata ya Old Moshi, katika jimbo la uchaguzi la Moshi vijijini wilayani hapa.

Katika kauli yake hiyo, Ngawaiya alisema hatua ya wananchi kuwapigia kura wapinzani ni kuwalimbikizia mali ambazo zinatokana na ruzuku ambayo chama kinapewa kwa ajili ya kujiendesha kwa kuwaendeleza wanachama wa chama husika.

Badala yake alisema, baadhi ya viongozi wa ngazi mbalimbali katika kambi ya upinzani wamekuwa wakitumia fedha za ruzuku kwa maslahi binafsi hususani katika kujikimu kimaisha.

Aliwataka wanachama kwa pamoja kuwa na mfumo wa mabadiliko ya kisiasa kwa kutizama upande wa pili wa kuipigia kura CCM,kwa kuzingatia kuwa kambi ya upinzani imeshikilia jimbo la Moshi vijijini kwa miaka kumi mfululizo bila ya maendeleo.

Pia alieleza kwamba wapinzani kwa sasa wameishiwa hoja za kuweza kuwaeleza wananchi kuwa nini watawafanyia na badala yake wamekuwa wakipiga kelele kwenye majukwaa ya kuipaka CCM matope.

Kwa upande mwingine alisema kuwa ameamua kurudi CCM,baada ya kubaini hali ilivyo katika vyama hivyo vya upinzani na kuahidi kumpigia debe mgombea wa ubunge Moshi vijijini Cyrill Chami.

Akielezea hatua ambayo ilimpelekea kujiunga na wapinzani kabla ya kurudi CCM, Ngawaiya aliwaambia wananchi hao kuwa alikuwa akitafuta njia mbadala ambayo ingewezesha kuratibu shughuli za kimaendeleo katika jimbo hilo lakini hali hiyo ilikuwa tofauti kutokana na kukosa ushirikiano na viongozi wa vyama vya upinzani.

Alipongeza hatua yake ya kujiunga na CCM kwa kile alichodai kuwa ni chama pekee ambacho kimekuwa madarakani kwa muda wote tangu enzi ya uhuru hivyo kuongeza kuwa chama kina uzoefu mkubwa na ndio chama kilichoweka mikakati ya maendeleo ambayo yameletwa kwa wananchi hadi sasa.

“Huwezi kuwa na kahawa bila kuwa na mapepe, na hivyo nchi haiwezi kuwa na  chama tawala bila upinzani na kwa hali hiyo kama mapepe ya kahawa hayawezi kuuzika na hayaendi sokoni vivyo hivyo na upinzani hauwezi kuingia Ikulu,” alieleza.

Katika mkutano huo umati mkubwa wa wanachama wa vyama vya upinzani vya kwenye kata hiyo walimkabidhi Ngawaiya fulana,  vitambaa na bendera za vyama vya upinzani ambapo aliwaahidi wanachama hao kuwa atawapa vipeperushi vya chama tawala kutokana na uamuzi wao huo wa kurejea CCM.

Hatua hiyo ya wanachama wa upinzani kurudi CCM ilikuwa ni pigo kwa kambi ya TLP ambapo Mwenyekiti wa tawi kupitia chama hicho kwenye kata hiyo Deoglas Kiwia alikuwa ni miongoni mwa wanachama waliorudisha bendera, katiba ya TLP na kadi.Kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kubariki ushindi wa kishindo wa CCM jimboni humo mwanachama huyo mpya wa CCM alimkabidhi mgombea ubunge wa CCM jimboni humo Dk.Chami fimbo kama ishara ya kuwa anayo nafasi kubwa ya ushindi na wanachama wa CCM wako tayari kumpigia kura Oktoba 30, mwaka huu.

 

Kampeni za Hawa Ghasia zasababisha matawi ya wapinzani kufungwa

Na Rashid Mussa, Mtwara

MGOMBEA ubunge kwa tiketi ya CCM Mtwara Vjijini, Hawa Ghasia ameonyesha umahiri mkubwa kwa kufagia kwa kiasi kikubwa upinzani kutokana na kuvuna mamia ya wanachama wapya kiasi cha kufanya baadhi ya matawi ya wapinzani kufungwa.

Hayo yamejitokeza katika kipindi cha wiki moja tu cha kampeni ya mgombea huyo iliyobatizwa jina la ‘kimbunga cha CCM’ ambacho juzi kiliingia katika kijii cha Mkunwa na kufanikiwa kuzoa wanachama wapya 50 na kufunga tawi la TLP kwa kukosa wanachama.

Uongozi uliokuwa wa tawi hilo ulikabidhi kwa Hawa bendera ya chama hicho na daftari la orodha ya wanachama wote na kadi zao.

Kimbunga hicho pia kimedhoofisha kabisa matawi kadhaa ya CUF katika Kata ya Mayanga na kutarajiwa kufungwa wakati wowote kutokana na wanachama na viongozi wao wengi kujiunga na CCM katika mkutano huo.

Kwa mujibu wa tathmini ya kampeni katika kipindi hicho cha wiki moja pia Kimbunga hicho kimedhoofisha kabisa matawi kadhaa ya CUF katika Kata ya Mayanga.

Wakati upinzani wilayani humo ukijawa na hofu ya kufagilia kabisa na mgombea huyo anayeonekana kukubalika hata na upinzani, nayo CCM inatumia mikutano yake kuvuna mamia ya wanachama wapya wanaojiunga kwa matumaini makubwa na uwakilishi ujao.

Katika mkutano wa uzinduzi rasmi wa kampeni hii uliofanyika kijiji  kilichokuwa kinaaminika kuwa CUF kumejichimbia cha Tangazo na kuhudhuriwa na maelfu ya watu, wananchi 100 walijiunga na CCM kati yao 26 kutoka upinzani.

Baadhi ya wananchi walisema Hawa amedhamiria kuwasaidia na ana uwezo na elimu ya juu ya mipango na uchumi hasa ukizingatiwa uzoefu wa utendaji kazi mzuri akiwa ofisa mipango wa wilaya iliyopiga hatua kubwa ya maendeleo mkoani hapa ya Masasi.

Katika kijiji cha Nyundo mara baada ya mkutano wa kampeni kumalizika watu 31 walijiunga na CCM kati yao 26 kutoka upinzani.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa George Mkuchika aliwaambia wananchi wa wilaya hiyo katika mkutano huo wa uzinduzi kuwa wasimpoteze mgombea huyo mwenye uwezo na msomi.

 

 

 

 

Hifadhi ya Wamimbiki yatoa milioni nne kusaidia ukarabati za zahanati

Na Prosper Kulita, Morogoro

HIFADHI ya Taifa ya Wamimbiki iliyopo wilayani Mvomero, Morogoroi imetoa msaada wa sh. milioni nne kwa ajili ya ukarabati wa zahanati ya Tarafa ya Kanga, katika jitihada za kusaidia shughuli za maendeleo ya jamii.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika kijiji cha Mziha, mgombea udiwani wa Kata ya

Kanga kupitia CCM,  Ramadhan Mhako, alisema fedha hizo zimetumika kukamilisha shughuli ambazo zilizokuwa

zimebaki.

Mhako alisema hifadhi hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kuleta maendeleo ya jamii katika vijiji vinavyozunguka ambavyo vimeunganisha wilaya mbili za

Mvomero mkoani Morogoro na Bagamoyo mkoani Pwani.

Mgombea ubunge wa jimbo la Mvomero, Suleiman Saddiq,  akizungumzia juu ya hifadhi hiyo wakati wa mkutano wa kampeni katika kijiji hicho, alisema asilimia 10 ya mapato yatakayotolewa na hifadhi hiyo baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu yatakuwa yakiingia katika Mfuko wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.

Alisema moja ya sababu ya kuingiza mapato hayo

kwa Wilaya ya Mvomero ni kutokana na wilaya hiyo kuunda halmashauri yake baada ya kumalizika Uchaguzi

Mkuu.

Fedha za mapato kutoka katika hifadhi pamoja na mapato mengine zilikuwa zikiingia katika Halmashauri

ya Wilaya ya Morogoro Vijijini ambayo mwaka 2003 imegawanywa na kuwa wilaya mbili ambazo ni

Morogoro Vijijini na Mvomero.

Alisema kuwa hata manufaa ya mapato mengine yaliyokuwa yakikusanywa katika vijiji vinavyounda wilaya hiyo yalikuwa  hayaonekani kutokana na kugawiwa katika

vijiji vingine ambavyo vilikuwa vinaunda wilaya ya Morogoro Vijijini.

Baada ya Mvomero kuunda halmashauri yake watapendekeza kiasi cha sh. million tatu kati ya zinazotolewa na hifadhi ya Wamimbiki zielekezwe katika miradi ya maji katika vijiji mbalimbali vya wilaya hiyo.

FGG yatoa sh. Milioni 139 kuboresha mazingira Tabora

Na El-hadji Yuusuf, Tabora

ASASI isiyokuwa ya kiserikali ya Forest Gadener Group (FGG) inatarajia kutumia sh. milioni 139 kwa ajili ya kusaidia shughuli za kuboresha mazingira katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Tabora, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa asasi hiyo, Davor Gamba, FGG inatarajia kufanya kazi ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya mazingira kwa raia, ukusanyaji wa habari kuhusu athari za mazingira na elimu ya mazingira mashuleni.

Alizitaja kazi nyingine zitakazofanywa na asasi hiyo ni pamoja na kuendesha semina kwa wadau wa mazingira katika mkoa huo ili kuweza kupunguza athari za mazingira, kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa usafi jinsi ya kupambana na ugonjwa wa malaria.

Gamba, alisema kuwa katika kupambana na malaria, asasi hiyo inatarajia kuwaelimisha watu hasa wale waishio vijijini mbinu za kupambana na ugonjwa huo na jinsi ya kuwaangamiza mbu.

Alisema asasi hiyo inatarajia pia kuendesha mradi wa kuotesha miti katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Tabora, ambayo athari za kukosekana kwa miti zimeanza kujitokeza.Aliongeza kuwa mradi huo unaanza kutekelezwa katika vijiji vya kata ya Igalula, ambapo asasi hiyo italazimika kuandaa vitalu kwa ajili ya kuotesha miche ya miti.

Pia alisema pamoja na kupanda miti, asasi hiyo imeanza kutoa elimu kwa wakazi wa kata hiyo jinsi ya kuzalisha mboga mboga na matunda ikiwa ni jitihada za kuwashirikisha katika mapambano dhidi ya umasikini.

Akiongea mara baada ya kufungua rasmi uendeshwaji wa mradi huo katika kata ya Igalula, Wilayani Uyui, Naibu Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi Tatu Ntimizi, alisema mradi huo utasaidia wakazi wa kata hiyo kujikwamua na umasikini.

Alisema kuwa FGG imeonyesha katika utekelezaji wa mradi huo utasaidia pia shughuli za kijamii kama ujenzi wa zahanati, ulezi wa wajane, wazee na watoto yatima, pamoja na kuwasaidia walemavu katika kukuza uchumi wao.

Naibu waziri huyo, alisema kuwa serikali itatoa msaada wa hali na mali katika kuhakikisha kuwa uendeshaji wa shughuli za asasi hiyo unafanyika bila vikwazo.

Mwenegoha aahidi kuendeleza huduma ya uji shuleni na hospitali

Na Latifa Ganzel, Morogoro

MGOMBEA Ubunge wa jimbo la Morogoro Kusini kwa tiketi ya CCM, Hamza Mwenegoha, amewaahidi watoto wa shule za

Msingi, wajawazito na waathirika wa ukimwiuwa akichaguliwa kuwa mbunge katika jimbo atahakikisha huduma ya uji inaendelea shuleni na hospitali.

Mwenegoha alisema hayo juzi alipokuwa akiongea na  wananchi wa jimbo hilo katika kampeni za  CCM.

Alisema amekuwa akitoa unga wa uji katika vituo vya afya na shule zote za msingi za jimbo hilo ili

kuwasaidia  wajawazito kupata uji wakiwa hospitalini na wanafunzi wakiwa mashuleni.

Aliongeza kuwa chakula hicho kimekuwa kikiwasaidia wajawazito hao ambao wengine ndugu zao wanakaa mbali

hivyo baada ya kujifungua wakipatiwa huduma hiyo ya chakula wanapata nguvu.

Mwenegoha alisema kwa upande wa shule, uji huo umekuwa ukiwasaidia watoto kuwa makini darasani na kuweza kusikiliza kwa makini walimu.

Alisema tangu kuanza kupatiwa uji kwa wanafunzi hao kumesaidia kwa kiasi kikubwa kuwapa fursa kuhudhuria vizuri masomo yao tofauti na ilivyokuwa awali.

Pia alisema imesaidia watoto wanaotoka umbali mrefu  kupata huduma hiyo na kuendelea  na masomo

badala ya kurudi nyumbani kwa ajili ya chakula cha mchana hali ambayo ilikuwa ikichangia kwa kiasi

kikubwa utoro.